Vyama na makundi mbalimbali yatia saini hati maalumu ya kisiasa nchini Sudan
(last modified Mon, 14 Nov 2022 06:29:33 GMT )
Nov 14, 2022 06:29 UTC
  • Vyama na makundi mbalimbali yatia saini hati maalumu ya kisiasa nchini Sudan

Vyama na makundi kadhaa ya kisiasa ambayo ni wanachama wa Muungano wa Uhuru na Mabadiliko wa Sudan yametia saini hati maalumu ya kisiasa inayokamilisha katiba mpya ya nchi hiyo

Kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim, Chama cha Ummah, Taasisi ya Ittihad, Baraza la Masuala ya Vyama vya Wafanyakazi Sudan, Muungano wa Kidemokrasia wa Asl na chama cha Congress ya Wananchi hivi karibuni walitia saini hati hiyo mpya ya kisiasa na inatarajiwa kuwa, vyama na taasisi nyingine za kisiasa zitatia saini hati hiyo karibuni hivi.

Kwa mujibu wa hati hiyo, amri na sheria zote zilizotolewa na kutekelezwa baada ya mapinduzi ya kijeshi dhidi ya serikali ya mpito ya Sudan zitafutwa na nchi hiyo itaongozwa katika kipindi cha mpito kwa mujibu wa katiba mpya.

Al Burhan, jenerali wa kijeshi aliyepandia mgongo wa maandamano ya wananchi kumpindua Omar al Bashir

 

Katiba mpya ya Sudan ya kipindi cha mpito inavipa haki vyama vinavyotia saini hati hiyo ya kisiasa, kuteua mawaziri wa serikali mpya, wajumbe wa baraza tawala, wabunge, magavana, mkuu wa idara ya mahakama na manaibu wake, pamoja na mkuu wa Mahakama ya Katiba.

Vyama na makundi yanavyotia saini hati hiiyo yanapaswa kuanzisha bunge huru ndani ya mwezi mmoja, ambalo wawakilishi wake hawapaswi kuwa zaidi ya watu 300. Bunge hilo litakuwa na jukumu la kutunga sheria, kusimamia vyombo vya utendaji na kuteua waziri mkuu.

Katiba mpya ya Sudan ilichapishwa kwa lengo la kuunda mfumo wa kidemokrasia wa mpito ili kumaliza mgogoro uliopo nchini humo. Sudan imeshuhudia mvutano mkubwa tangu yalipotokea mapinduzi ya kijeshi ya Oktoba 25 yaliyofanywa na mkuu wa jeshi Abdul Fattah al-Burhan.

Tags