Dec 02, 2022 02:44 UTC
  • Askari wa Tanzania, Botswana wauawa Cabo Delgado, Msumbiji

Wanajeshi wawili wa kikosi cha Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika SADC wameuawa katika makabiliano baina yao na wanamgambo katika jimbo la Cabo Delgado kaskazini mwa Msumbiji.

Taarifa ya kikosi hicho cha kieneo kinachojulikana kwa kifupi kama SAMIM imesema, wanajeshi hao wawili waliouawa ni Sajenti Musa Mpondo wa Jeshi la Wananchi Tanzania na Koplo Zikamee Kamai wa Jeshi la Ulinzi la Botswana.  

Aidha wanamgambo 30 wanaoaminika kuwa wanachama wa kundi la kigaidi linalojiita Ahlu Sunna Wal Jamaa (ASWJ) wamengamizwa katika makabiliano hayo yaliyotokea Jumanne katika kijiji cha Nkonga, wilaya ya Nangade.

Kikosi cha kieneo cha SAMIM kimefanikiwa kutwaa silaha na zana za kivita zilizokuwa mikononi mwa magaidi hao wenye mfumgamano na genge la kigaidi la ISIS.

Profesa Mpo Molomo, mkuu wa kikosi hicho kinachoundwa na nchi nane wanachama wa jumuiya ya kieneo ya SADC amesema magaidi waliouawa katika makabiliano hayo wanapindukia 30, huku wengine wengi wakijeruhiwa.

Ramani inayoonesha jimbo la Cabo Delgado kaskazini mwa Msumbiji

Jimbo tajiri kwa nishati ya gesi la Cabo Delgado kaskazini mwa Msumbiji limekumbwa na machafuko na hujuma za wanamgambo wenye mfungamano na kundi la kigaidi la Daesh tangu mwishoni mwa mwaka 2017.

Makumi ya maelfu ya watu wameuliuwa na kujeruhiwa katika hujuma za wanamgambo hao na wengine laki nane wamelazimika kuhama makazi yao.

Tags