Ripoti: Askari wa Eritrea wangali wanaua raia Tigray, Ethiopia
(last modified Sat, 03 Dec 2022 10:26:42 GMT )
Dec 03, 2022 10:26 UTC
  • Ripoti: Askari wa Eritrea wangali wanaua raia Tigray, Ethiopia

Jeshi la Eritrea linatuhumiwa kuwa linaendelea kufanya mauaji ya raia katika eneo la Tigray, kaskazini mwa Ethiopia.

Takwimu mpya za Kituo cha Dharura cha Tigray zimefichua kuwa, raia 111 wameuawa na wanajeshi wa Eritrea ambao wanapigana bega kwa bega na askari wa Ethiopia huko mashariki mwa Tigray, baina ya Novemba 17 na 25 mwaka huu.

Aidha kwa mujibu wa ripoti hiyo, raia wengine 103 wamejeruhiwa kwenye operesheni za jeshi la Eritrea, huku raia 39 wakitoweka na nyumba zaidi ya 240 zikiteketezwa kwa moto katika kipindi hicho.

Mamlaka za kieneo huko Tigray, asasi za Umoja wa Mataifa na asasi zisizo za serikali zimeshiriki katika ukusanyaji wa takwimu hizo za Kituo cha Dharura cha Tigray.

Weledi wa mambo wanasema, mashambulizi hayo ya wanajeshi wa Eritrea yanatishia makubaliano yaliyofikiwa Novemba 2 kati ya serikali ya Ethiopia na wapiganaji wa harakati ya kupigania ukombozi wa eneo la Tigray TPLF. Eritrea haikushiriki kwenye mazungumzo hayo ya amani yaliyofanyika nchini Afrika Kusini.

Umoja wa Mataifa umekuwa ukisisitiza mara kwa mara kuwa, askari wa Eritrea wanapaswa kukomesha ukatili na vitendo viovu katika eneo la Tigray nchini Ethiopia na kuondoka mara moja katika eneo hilo.

Hivi karibuni pia, shirika la kutetea haki za binadamu la Amesty International lilitangaza kuwa jeshi la Eritrea limefanya mauaji ya umati katika eneo hilo la Tigray. Aidha Human Rights Watch (HRW) ilisema  karibuni kuwa askari wa Eritrea wameua mamia ya raia wakiwemo watoto wadogo katika eneo hilo la kaskazini mwa Ethiopia.