Pande hasimu nchini Sudan kusaini makubaliano ya kisiasa
(last modified Sat, 03 Dec 2022 11:55:56 GMT )
Dec 03, 2022 11:55 UTC
  • Pande hasimu nchini Sudan kusaini makubaliano ya kisiasa

Makundi ya kiraia na utawala wa kijeshi unaongoza hivi sasa nchini Sudan zinatazamiwa kusaini makubaliano ya kisiasa Jumatatu ijayo, kwa shabaha ya kuhitimisha mgogoro wa kisiasa wa nchi hiyo.

Makubaliano hayo yatajumuisha Vikosi vya Uhuru na Mabadiliko (FFC), Chama cha Kongresi (PCP), Chama cha Muungano wa Kidemokrasia (DUP) na Jukwaa la Mapinduzi la Wasudan (RSF).

Harakati ya kisiasa ya FFC imesema kuwa, mapatano hayo ya amani yatatumiwa kama msingi wa utawala wa kiraia na kuundwa kwa serikali ya mpito nchini humo.

FFC imesema makubaliano hayo ya kisiasa yaliyofikiwa kutokana na jitihada za Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya, Imarati, Saudi Arabia, Uingereza na Marekani yatasainiwa Jumatatu ijayo.

Hata hivyo mapatano hayo yamepingwa na kukosolewa na Chama cha Wanataaluma wa Sudan (SPA), Chama cha Kikomunisti na makundi mengie madogo ya kisiasa ya nchi hiyo.

Makubaliano ya amani ya Sudan mwaka 2020

Katika miezi ya karibuni, Sudan imekumbwa na maandamano yaliyotawaliwa na fujo na machafuko makubwa kutokana na mapinduzi ya kijeshi yaliyofanywa Oktoba 25, 2021 dhidi ya serikali ya kiraia iliyokuwa ikiongozwa na Waziri Mkuu Abdallah Hamdok.

Waandamanaji nchini humo wamekuwa wakisisitiza juu ya kurejeshwa kwa utawala wa kiraia, huku baadhi yao wakiandamana kupinga uingiliaji wa nchi za kigeni katika masuala ya ndani ya nchi yao.

Tags