Raia wa Italia anayeaminika kuwa Daesh akamatwa Morocco
Vyombo vya usalama nchini Morocco vimesema kuwa vimemtia nguvuni raia wa Italia anayeaminika kuwa na mafungamano na kundi la kigaidi la Daesh.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Morocco leo Jumatatu imesema kuwa, raia huyo wa Italia ambaye amekuwa akiishi Ubelgiji amekamatwa katika uwanja wa ndege wa Oujda karibu na mpaka wa nchi hiyo na Algeria. Taarifa hiyo imeongeza kuwa, raia huyo wa Italia alitumwa na magaidi wa ISIS yaani Daesh kwenda kufanya mashambulizi huko Casablanca, mji mkuu wa kibiashara wa Morocco.
Mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Morocco ilisema kuwa, polisi imewatia mbaroni watu tisa katika miji mbalimbali ya nchi hiyo walipokuwa wakipanga shambulio la kigaidi. Katika ripoti hiyo, magaidi hao walikuwa wanakusudia kwenda Libya kwa ajili ya kujifunza mafunzo ya kijeshi.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya serikali, raia zaidi ya 2,000 wa Morocco wamejiunga na kundi la Daesh hadi kufikia sasa, ambapo 246 miongoni mwao wameuawa nchini Syria, 40 Iraq huku 156 wakiliasi kundi hilo na kurejea nnchini kwao Morocco.