Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akaribisha makubaliano ya makundi ya Sudan
(last modified Tue, 06 Dec 2022 02:57:44 GMT )
Dec 06, 2022 02:57 UTC
  • Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akaribisha makubaliano ya makundi ya Sudan

Antonio Guterres Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekaribisha na kuunga mkono kusainiwa makubaliano kati ya makundi ya kiraia ya kisiasa na jeshi la Sudan kwa ajili ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa nchini humo.

Makundi ya kiraia na jeshi la Sudan jana yalitia saini makubaliano hayo katika ikulu ya rais mjini Khartoum kwa shabaha ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa wa nchi hiyo. Abdulfattah al Burhan Mkuu wa baraza la utawala la Sudan na Naibu wake Mohamed Hamdan Dagalo maarufu kama Hemeti, na shakhsia kadha wa kisiasa na kidiplomasia kutoka nchi za Ulaya na Kiarabu walihudhuria utiaji saini wa makubaliano hayo tajwa. 

Mohamed Hamdan Dagalo na Jenerali Abdulfattah al Burhan 

Kwa mujibu wa makubaliano hayo ambayo yana vipengee vitano vikuu ikiwa ni pamoja na kanuni jumla; shaksia kutoka kundi la kiraia ndiye atakayeongoza masuala na majukumu ya kipindi cha mpito, miundo ya madaraka wakati wa kipindi cha mpito, taasisi za kawaida n.k. 

Aidha kwa mujibu wa makubaliano hayo, Waziri mkuu wa mpito atachaguliwa kuhudumu kwa kipindi cha miaka miwili na vikosi vya mapinduzi ambavyo vimetia saini makubaliano hayo. Makubaliano hayo aidha yanaeleza kuwa, vikosi vya kukabiliana na radimali ya haraka vinapasa kuunganishwa na vikosi vya jeshi vya Sudan katika muda fulani na kusiundwe kundi lolote la wanamgambo nchini humo. 

Tags