Matukio ya Sudan na onyo la Harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo
(last modified Sat, 10 Dec 2022 02:15:21 GMT )
Dec 10, 2022 02:15 UTC
  • Matukio ya Sudan na onyo la Harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo

Makubaliano ya kusuluhisha mgogoro wa kisiasa wa Sudan yametiwa saini na vyama vya kisiasa vya nchi hiyo katika hali ambayo wengi wana wasiwasi kuhusu mustakabali wa nchi hiyo na uingiliaji wa nchi za kigeni katika mambo ya ndani ya nchi hiyo ya Kiafrika.

Kuhusiana na suala hilo, Ali Ahmed Karti, Katibu Mkuu wa Harakati ya Kiislamu ya Sudan ametahadharisha kuhusu matokeo mabaya ya utegemezi wa nchi hiyo kwa wageni jambo linalochochea ukosefu wa usalama katika eneo. Akiashiria kwamba kujishughulisha na masuala ya kisiasa ni haki ya kimsingi ya kila raia wa Sudan, Katibu Mkuu wa Harakati ya Kiislamu ya Sudan ametaka kuwepo maridhiano ya kitaifa ambayo yatajumuisha nyanja zote za kisiasa na kijamii bila ya upendeleo au ubaguzi, ili kipindi cha mpito kiweze kujumuisha marekebisho yanayokusudiwa ya kisiasa.

Tangu Oktoba 2021 na kufuatia mapinduzi ya kijeshi katika nchi hiyo, Sudan imekuwa ikikabiliwa na mzozo wa kisiasa ambao umesababishwa na kuendelea kuwepo wanajeshi katika kileleni cha madaraka nchini. Kinyume na matakwa ya wananchi, jeshi limeendelea kusalia madarakani baada ya kufanya mapinduzi. Hii ni pamoja na ukweli kwamba watu wa nchi hiyo, na hasa katika mwaka uliopita, wamekuwa wakifanya mikutano ya malalamiko na maandamano, wakitaka raia wakabidhiwe madaraka kwa njia ya amani.

Ali Ahmed Karti

Kufuatia kushadidi mgogoro wa kisiasa huko Sudan ambao umesababishwa na kuongezeka uingiliaji wa kigeni nchini, katika siku chache zilizopita, makundi ya kiraia na baraza tawala la kijeshi la Sudan wametia saini makubaliano ya kutatua mgogoro huo wa kisiasa. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, makundi ya kiraia na wanajeshi wamekubaliana kuhusu kipindi cha mpito cha miezi 24 ambacho kitaanza wakati waziri mkuu wa mpito atakapochaguliwa.

Licha ya kutiwa saini mkataba huo, makundi mengi ya kisiasa yana wasiwasi kuhusu mashinikizo ya nchi za kigeni na uingiliaji wao katika masuala ya ndani ya nchi hiyo. Waandamanaji wengi wametoa wito wa kukomeshwa uingiliaji huo kwa kauli mbiu zinazosema "Hatutaki ukoloni mamboleo", "Hatutaki uingiliaji wa kigeni katika masuala ya ndani ya Sudan" na "Sudan ni nchi huru." Kwa hakika kuendelea kuwa na nguvu wanajeshi wa Sudan kumepelekea ushawishi na uingiliaji wa nchi za kigeni hususan Saudi Arabia na utawala wa Kizayuni kuongezeka nchini humo; kinyume kabisa na matakwa ya Wasudani. Ni kwa msingi huo ndipo hata wakataka kufukuzwa kwa Volker Perthes, mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo.

Wasudan wanaamini kuwa wanaweza kutatua matatizo yao bila kuingiliwa na balozi za kigeni mjini Khartoum. Hii ni katika hali ambayo nchi na mashirika mengi ya kimataifa yamewasilisha mipango mbalimbali kwa kisingizio cha kurudisha amani na kutatua mgogoro wa kisiasa wa Sudan na kuitaka serikali ya Khartoum ifuate siasa zao kuhusu jambo hilo. Waandamanaji wa Sudan wanasema lengo la wageni ni kutaka kuwadhibiti watu wa Sudan na kutumia vibaya masuala na matatizo yao kwa manufaa yao wenyewe.

Mgogoro wa kisiasa wa Sudan umepamba moto katika hali ambayo miezi kadhaa iliyopita, na kinyume na ahadi zilizotolewa na serikali, hali ya uchumi ya nchi hiyo imezidi kuzorota, na umaskini na ukosefu wa ajira kuongezeka maradufu, mambo mawili ambayo ndiyo yaliyosababisha mapinduzi ya wananchi dhidi ya utawala wa Rais Omar al-Bashir!

Abdel Fattah al-Burhan, mtawala wa kijeshi wa Sudan

Adel Ahmad Ismail, mjumbe wa Muungano wa Maabara ya Matibabu wa Sudan amebainisha kuwa lengo ni kufichua madai ya uongo ya serikali ambayo haitekelezi ahadi zake na kusema: Mapinduzi ni mapinduzi ya wananchi na tunafuatilia malengo ya mapinduzi kwa njia ya amani.

Raia wengi wa Sudan wanatumai kutekelezwa makubaliano yaliyotiwa saini karibuni kwa ajili ya kufikia amani na hatimaye kuondoka wanajeshi madarakani. Pamoja na hayo lakini vyama na raia wengine wa nchi hiyo wangali wana wasiwasi kuhusu jinsi makubaliano hayo yatakavyotekelezwa kwa mafanikio. Bado wana wasi wasi kuhusu kuendelea uingiliaji wa kigeni katika mambo ya ndani ya nchi yao na kutumiwa vibaya nchi hiyo kwa mslahi ya wageni. Onyo la Katibu Mkuu wa Harakati ya Kiislamu ya Sudan pia linapaswa kutathminiwa katika mtazamo huo.

Kwa vyo vyote vile, siku zijazo zinaonekana kuwa muhimu sana kwa taifa la Sudan.

Tags