Morocco yapanga safari 30 za ndege kuwabeba mashabiki hadi Doha
(last modified Tue, 13 Dec 2022 04:32:10 GMT )
Dec 13, 2022 04:32 UTC
  • Morocco yapanga safari 30 za ndege kuwabeba mashabiki hadi Doha

Shirika la Ndege la Morocco, Royal Air Maroc linapanga safari 30 za ndege maalum kuwabeba mashabiki wa soka kutoka Casablanca hadi Doha kwa mchezo wa Jumatano wa nchi hiyo wa nusu fainali ya Kombe la Dunia dhidi ya Ufaransa.

Katika taarifa Jumatatu, shirika hilo la ndege lilisema ndege hizo zitaondoka leo Jumanne na mapema kesho Jumatano.

Morocco imekuwa ya kwanza barani Afrika kufuzu kwa nusu fainali ya Kombe la Dunia.

Abiria hao wataongeza kwa maelfu raia wa Morocco ambao tayari wanahudhuria mashindano ya soka huko Doha.

Timu ya soka ya taifa ya Morocco iliweza kusonga mbele katika nusu fainali ya Kombe la Dunia siku ya Jumamosi kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ureno na kumuacha gwiji wa soka Cristiano Ronald na wenzake wakigaragara kwa vilio na majonzi.

Bao la ushindi lilifungwa dakika za mwisho za kipindi cha kwanza wakati Youssef En-Nesyri alipoteleza na kushinda kwa kichwa krosi iliyopigwa na Yahya Attiat-Allah. Kipa wa Portugal Diogo Costa alijaribu kumzuia En-Nesyri kwa krosi lakini En-Nesyri alimruka kila mmoja na kuutumbukiza mpira wavuni.

Mashabiki wa soka kote Afrika na katika nchi za Kiarabu wana matumaini makubwa kuwa Morocco itaweza kufuzu na kuingia fainali ya Kombe la Dunia mwaka huu.