Libya: Hatutaruhusu kufunguliwa tena kwa kesi ya Lockerbie
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i91758
Waziri Mkuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya ametangaza kuwa nchi hiyo haitaruhusu kesi ya Lockerbie kufunguliwa tena.
(last modified 2025-07-26T11:21:05+00:00 )
Dec 16, 2022 08:04 UTC
  • Abdul Hamid al-Dbeibeh
    Abdul Hamid al-Dbeibeh

Waziri Mkuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya ametangaza kuwa nchi hiyo haitaruhusu kesi ya Lockerbie kufunguliwa tena.

Abdul Hamid al-Dbeibeh amesema kuwa jukumu la nchi hiyo kwa kadhia ya Lockerbi limekwisha na kwamba hataruhusu kesi hiyo kufunguliwa tena.

Matamshi ya Dbeibeh yanakuja baada ya maafisa wa serikali za Scotland na Marekani kutangaza Jumapili iliyopita kwamba Mlibya anayetuhumiwa kutengeneza bomu lililosababisha mlipuko wa ndege ya Pan Am kwenye anga ya Lockerbie, Scotland mwaka 1988 yuko kizuizini nchini Marekani. 

Abu Agila Mohammad Mas'ud Kheir Al-Marimi amekamatwa karibu miaka miwili baada ya Mwanasheria Mkuu wa Marekani, Bill Barr, kutangaza kwa mara ya kwanza kwamba Washington inamtuhumu kuhusika na faili la Lockerbie. 

Ndege ya Pan Am, Boeing 747, iliripuka ikiwa juu ya mji mdogo wa Lockerbie, Scotland, na kuwauwa watu 259 waliokuwemo ndani yake na wengine 11 mahala ilipoangukia.

Wakati huo huo, Wizara ya Sheria ya Marekani hivi karibuni ilitangaza kwamba Abu Agila Muhammad al-Marimi amekamatwa baada ya miaka 34.

Abu Agila Mohammad (katikati)

Ingawa maafisa wa Marekani hawajatoa maelezo kuhusu jinsi Abu Agila alivyokamatwa, ilitangazwa mwezi uliopita kuwa watu wenye silaha walimteka nyara kutoka kwa nyumbani kwake huko Tripoli.