Comoro yatazamiwa kuchukua uenyekiti wa Umoja wa Afrika
Rais Azali Assoumani wa Comoro anatazamiwa kuwa mwenyekiti mpya wa Umoja wa Afrika mwaka ujao 2022, baada ya Rais William Ruto wa Kenya kujiondoa kwenye kinyang'anyiro cha kuwania nafasi hiyo.
Visiwa hivyo ambavyo vinapatikana katika bahari ya Hindi mashariki mwa Afrika vitakuwa vya kwanza kutwaa uenyekiti wa taasisi hiyo kubwa ya kibara.
Dakta Ruto hivi karibuni alitangaza kujiondoa kwenye mchuano wa kumtafuta mwenyekiti mpya wa AU, na hivyo kumuandalia mazingira Rais wa Comoro kuchukua nafasi hiyo ambayo mara hii sharti ichukuliwe na kiongozi wa Afrika Mashariki.
Serikali ya Comoro imepokea kwa mikono miwili habari hiyo ya kujiondoa Ruto kwenye kinyang'anyiro hicho na kumpa ahueni Rais Azali Assoumani.
Taarifa ya serikali ya Comoro imesema: Rais Azali Assoumani ametoa shukrani za dhati kwa kuwa alifuatilia kwa unyenyekevu tangazo la ndugu William Ruto, Rais wa Jamhuri ya Kenya la kujiondoa kwenye mchuano wa kuwania urais wa Umoja wa Afrika kwa mwaka 2023.

Duru za habari zinaarifu kuwa, kujiondoa Kenya na kuipisha Comoro kulichukua jitihada za kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili, huku mwenyekiti wa sasa, Macky Sall, Rais wa Senegal akihusishwa pia kwenye lobi hizo.
Ikumbukwe kuwa, Rais Azali Assoumani alipata asilimia 59 ya kura katika uchaguzi wa urais uliofanyika mwezi Machi mwaka 2019 nchini Comoro. Mwaka mmoja kabla, Rais Assoumani alishinda kura ya maoni ya marekebisho ya katiba ya kurefusha kipindi cha uongozi wa rais na kukomesha mfumo wa kuongoza kwa zamu baina ya visiwa vitatu vikuu vinavyounda Jamhuri ya Watu wa Comoro.