Wataalamu: Kuomba radhi hakutoshi, Uholanzi iifidie Afrika kwa utumwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i92042-wataalamu_kuomba_radhi_hakutoshi_uholanzi_iifidie_afrika_kwa_utumwa
Wataalamu, wanaharakati na wasomi wa Afrika wamesema haitoshi kwa nchi Magharibi kuomba radhi kwa kufanya biashara haramu ya utumwa na jinai nyinginezo katika enzi za ukoloni, na badala yake zinapaswa kuzifidia nchi zilizoathiriwa na jinai hizo.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
Dec 24, 2022 02:35 UTC
  • Wataalamu: Kuomba radhi hakutoshi, Uholanzi iifidie Afrika kwa utumwa

Wataalamu, wanaharakati na wasomi wa Afrika wamesema haitoshi kwa nchi Magharibi kuomba radhi kwa kufanya biashara haramu ya utumwa na jinai nyinginezo katika enzi za ukoloni, na badala yake zinapaswa kuzifidia nchi zilizoathiriwa na jinai hizo.

Kealeboga Maphunye, Profesa wa Sayansi ya Afrika katika Chuo Kikuu cha Afrika Kusini amesema hatua ya nchi za Magharibi kuomba radhi bila kutoa fidia ya maana kwa waathiriwa wa jinai za utumwa na ukoloni ni ya kimaonyesho, na ambayo haiwezi kuwaondolea au hata kuwapunguzia machungu waathiriwa wa jinai hizo.

Haya yanajiri siku chache baada ya Mark Rutte, Waziri Mkuu wa Uholanzi kuomba radhi kwa niaba ya serikali ya nchi hiyo kutokana na taifa hilo kuhusika na biashara haramu ya utumwa huko nyuma. Katika kikao na waandishi wa habari mjini Hague Jumatatu iliyopita, Waziri Mkuu wa Uholanzi alidai kuwa, "Tunaweza kuutambua utumwa kwa njia ya wazi zaidi kama jinai dhidi ya binadamu."

Profesa Maphunye amesema, "Afrika Kusini, kwa mfano, tangu Waholanzi walipowasili nchini hapa mwaka 1652, tungali tunahisi athari za utumwa hadi leo hii."

Naye Mustafa Mheta, mtafiti na Mkuu wa Dawati la Afrika katika taasisi ya wanafikra ya Media Review Network yenye makao yake jijini Johannesburg amesema, "Afrika haiwezi kufikia maridhiano na Magharibi katika suala la utumwa, hadi pale Waafrika watakapoombwa radhi na nchi za Magharibi zilizonunua watumwa (wa Kiafrika), na kulilipa fidia bara la Afrika."

Wanaharakati wa Kiafrika wamekosoa kauli ya Waziri Mkuu wa Uholanzi kwamba nchi hiyo haitatoa fidia kwa vizazi vya wahanga wa utumwa barani Afrika, na badala yake, serikali ya nchi hiyo itatenga dola milioni 212 kwa ajili ya 'mipango' ya kukabiliana na kumbukumbu ya utumwa iliyobakia nchini humo na katika makoloni yake ya zamani.