Gharama za maisha zapanda pakubwa Nigeria huku watu maskini wakiongezeka nchini
Kitengo cha Taifa cha Takwimu nchini Nigeria kimetangaza kuwa gharama za maisha zimeongezeka huku jamii ya watu maskini ikiongezeka pia nchini humo.
Kitengo cha Taifa cha Takwimu cha Nigeria kimeeleza kuwa, gharama za maisha zimeongezeka sana nchini humo kiasi kwamba watu wasiopungua milioni 135 wanakabiliwa na umaskini katika nyanja mbalimbali. Kwa mujibu wa takwimu hizo, raia wa Nigeria hutumia karibu nusu ya mapato yao kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya familia.
Hii ni katika hali ambayo, bei za bidhaa mbalimbali za chakula zimeongezeka pakubwa ambapo hivi sasa katika kukaribia Sikukuu ya Mwaka Mpya, aghalabu ya wananchi wa Nigeria hawana uwezo wa kufanya safari za kuwatembelea ndugu na jamaa zao.
Hali hii tajwa inaripotiwa kuwa mbaya sana na kuwaathiri pakubwa wale ambao wanapanga nyumba kwa sababu nyumba za kupanga zimepanda sana katika miaka ya karibuni huko Nigeria. Nusu ya watu milioni 200 ambayo ni jamii nzima ya NIgeria wanaishi kwa pato la chini ya dola mbili kwa siku.