Watu wasiopungua 16 wamepoteza maisha katika ajali ya basi huko Omdurman, Sudan
Basi ya abiria mapema leo liligonga lori lililokuwa limeegeshwa katika barabara kuu kwenye mji wa Omdurman huko Sudan na kuuwa watu wasiopungua 16.
Taarifa ya polisi imeeleza kuwa, basi hilo liliacha njia na kugonga lori lililokuwa limeegeshwa huko Omdurman, mji pacha wa mji mkuu wa Sudan Khartoum. Watu wengine wasiopungua 19 wamejeruhiwa kwenye ajali hiyo.
Basi hilo lililokuwa na abiria lilikuwa likitoka katika mji wa Fasher kuelekea Khartoum. Magari ya kubebea wagonjwa yalifanikiwa kufika haraka katika eneo la ajali na kuwachukua majeruhi hadi katika hospitali ya Omdurman kwa ajili ya kupatiwa matibabu. Miili ya abiria walioaga dunia ilipelekwa mochwari kuhifadhiwa kabla ya kukabidhiwa na ndugu zao.
Ajali za barabarani zimekuwa zikishuhudiwa mara kwa mara huko Sudan; nyingi miongoni mwao zikiwa ni matokeo ya barabara mbovu na utekelezaji duni wa sheria za trafiki. Maelfu ya watu hupoteza maisha kila mwaka kwa ajali za barabarani nchini Sudan.