UN yaidhinisha kupanuliwa operesheni za EU, Libya
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa sauti moja limepasisha azimio linaloupa idhini Umoja wa Ulaya kuongeza operesheni za vikosi vyake vya majini katika pwani ya Libya, katika Bahari ya Mediterranean.
Rasimu ya azimio hilo iliandaliwa na Uingereza na Ufaransa kwa shabaha ya kuviruhusu vikosi vya Umoja wa Ulaya katika pwani ya Libya kukamata silaha haramu katika operesheni iliyopewa jina la 'Operation Sophia'.
Francois Delattre, mkuu wa hivi sasa wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa raia wa Ufaransa amesema kupitia azimio hilo kwamba sasa itakuwa rahisi kutekeleza vikwazo vya silaha dhidi ya Libya. Tayari manowari za EU zimetumwa katika pwani ya Libya kuwakamata wahamiaji wanaotaka kuingia bara Ulaya wakiwa wamejizatiti kwa silaha.
Wiki iliyopita, Martin Kobler, Mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya alilimbia Baraza la Usalama kuwa, kuna silaha milioni 20 katika nchi hiyo ya Kaskazini mwa Afrika yenye idadi ya watu milioni 6.
Wahajiri karibu laki mbili wameingia Ulaya kupitia Bahari ya Mediterranean katika mwaka huu pekee huku wengine 2,000 wakifariki dunia kwa kuzama baharini.