Wafadhili waahidi dola bilioni 30 kwa ajili ya kilimo barani Afrika
(last modified Sat, 28 Jan 2023 11:49:05 GMT )
Jan 28, 2023 11:49 UTC
  • Wafadhili waahidi dola bilioni 30 kwa ajili ya kilimo barani Afrika

Washirika wa maendeleo wa Afrika wameahidi kutoa dola bilioni 30 kwa maendeleo ya kilimo na uhuru wa chakula kwa bara hilo katika miaka mitano ijayo.

Tangazo hilo lilitolewa jana Ijumaa wakati wa kufungwa kwa mkutano wa kilele wa chakula Afrika katika mji mkuu wa Senegal, Dakar.

Ufadhili huo utajumuisha msaada wa moja kwa moja katika utoaji wa pembejeo za kilimo.

Katika taarifa yao, viongozi walioshiriki wamepongeza, "uwekezaji uliopangwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika wa dola bilioni 10 na dola bilioni 20 zaidi na washirika wengine kadhaa katika kuunga mkono mabadiliko ya kilimo barani Afrika."

Viongozi hao pia walijitolea tena kuongeza ufadhili kutoka kwenye bajeti ya kitaifa kwa ajili ukuaji wa kilimo na mabadiliko kwa ustawi wa pamoja na kuboresha maisha kwa kutenga angalau 10% ya matumizi ya umma kwa ajili ya kilimo.

Mkutano huo wa siku tatu ulipendekezwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika kujadili hatua madhubuti za kulisha karibu watu milioni 250 wanaokabiliwa na njaa barani Afrika.

Afrika ina asilimia 65 ya ardhi ya dunia iliyosalia isiyolimwa na ina uwezo wa kuzalisha chakula cha kutosha kujilisha yenyewe na kuchangia kulisha dunia nzima.

Lakini licha ya uwezo wake mkubwa wa kilimo, Afrika inakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, ambapo thuluthi moja ya watu milioni 828 wana njaa katika baŕa hilo.

Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Akinwumi Adesina alisema katika mkutano huo kwamba kinachofanywa na Afiika katika kilimo kitaamua ugavi wa chakula duniani. "Dunia nzima itaunga mkono Afrika katika kufikia malengo yake", amesema Akinwumi Adesina.

Viongozi wa nchi na serikali za nchi 34 za Afrika, wakuu wa mashirika ya maendeleo ya kimataifa na baina ya nchi na viongozi wa sekta ya kibinafsi walihudhuria mkutano huo ulioandaliwa na Rais wa Senegal na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Macky Sall.

Tags