Chad yakanusha kuwaua raia katika mashambulizi ya anga dhidi ya wanamgambo
Serikali ya Chad imekanusha vikali ripoti kwamba jeshi lake liliwashambulia raia katika operesheni dhidi ya wanamgambo wanaobeba silaha.
Duru za ndani za Chad zimearifu kuwa makumi ya wavuvi katika nchi jirani ya Nigeria wameuawa katika mashambulizi ya anga ya jeshi la Chad.
Jeshi la Chad Jumatano iliyopita lilitekeleza mashambulizi ya anga na kukipiga kisiwa cha Tilma katika wilaya ya Kukawa upande wa nchi jirani ya Nigeria katika Ziwa Chad ikiwa ni katika kujibu mashambulizi ya kundi la kigaidi la Boko Haram dhidi ya kambi ya jeshi la Chad ambapo askari wasiopungua 40 waliuawa.
Abderaman Koulamallah Msemaji wa serikali ya Chad amesema kuwa wanakanusha vikali ripoti za hivi karibuni kwamba jeshi ya nchi hiyo limewashambulia raia, hasa wavuvi katika eneo la Ziwa Chad.
"Operesheni zilizotekelezwa hadi sasa na jeshi la Chad zimeyalenga makundi ambayo waliyabaini vyema", amesema Msemaji wa serikali ya Chad.