Israel yaendeleza mashambulio ya kiwendawazimu Ghaza
(last modified Tue, 20 May 2025 06:54:15 GMT )
May 20, 2025 06:54 UTC
  • Israel yaendeleza mashambulio ya kiwendawazimu Ghaza

Duru za habari za ndani ya Palestina zimeripoti mapema leo Jumanne kwamba ndege za kivita za Israel zimefanya mashambulizi makali na ya kiwendawazimu katika maeneo mbalimbali ya mji wa Ghaza.

Mapema leo Jumanne, duru za habari za ndani ya Palestina zimeonesha mikanda ya video inayohusiana na mashambulizi makali ya ndege za kivita za jeshi katili la Israel, kwenye maeneo mbalimbali ya mji wa Ghaza.

Televisheni ya Al-Mayadeen imeripoti kuwa: "Ndege za dola vamizi la Kizayuni, zimefanya kwa uchache mashambulizi 10 katika kitongoji cha Al-Tuffah mashariki mwa Mji wa Ghaza na sehemu ya mashariki ya Jabalia, huko kaskazini mwa Ukanda wa Ghaza."

Mwandishi wa Al-Mayadeen aliyeko kwenye Ukanda wa Ghaza amesema: "Shambulio la utawala vamizi wa Israel katika skuli ya Musa bin Nasir, ambayo ilikuwa makazi ya wakimbizi wa Palestina kwenye kitongoji cha Al-Darj mashariki mwa Mji wa Ghaza, limewateketeza kabisa wakimbizi wa Kipalestina waliokuwepo hapo."

Ripoti hiyo pia imeeleza kuwa, ndege za kivita za Israel zimeshambulia kwa mabomu majengo ya makazi ya watu katika mji wa Deir al-Balah katikati mwa Ukanda wa Ghaza.

Kwa upande wake, televisheni ya Al Jazeera ya Qatar imeiripoti kuwa, kwa uchache Wapalestina 12 wameuawa shahidi na wengine wengi hawajapatikana hadi hivi sasa na hawajulikani hatima yao kutokana na mashambulizi ya dola vamizi la Israel kwenye eneo la Deir el-Balah.