Walimwengu wazidi kuishinikiza Israel ivunje mzingiro dhidi ya Gaza
(last modified Tue, 20 May 2025 13:25:08 GMT )
May 20, 2025 13:25 UTC
  • Walimwengu wazidi kuishinikiza Israel ivunje mzingiro dhidi ya Gaza

Mataifa mbalimbali ya dunia yameendelea kutoa mwito kwa utawala haramu wa Israel ili uhitimishe mzingiro wake dhidi ya Ukanda wa Gaza.

Zaidi ya nchi 20 zimetoa wito kwa utawala wa Israel kuruhusu mara moja urejeshaji kamili wa utoaji wa misaada huko Gaza.

Zaidi ya nchi 20 ukiwemo Umoja wa Ulaya zimeutaka utawala wa Israel kuondoa vikwazo vya kupeleka misaada katika Ukanda wa Gaza na kuruhusu Umoja wa Mataifa na mashirika ya kibinadamu kufanya kazi zao kwa uhuru na bila upendeleo.

Katika taarifa yao ya pamoja, mawaziri wa mambo ya nje kutoka nchi kama Australia, Canada, Japan na Ufaransa wamesisitiza kwamba wakazi wa Gaza wanakabiliwa na hatari ya njaa na kwamba, watu wa eneo hilo lazima wapate misaada muhimu mara moja.

Taarifa hiyo imesisitiza kuwa, kanuni na misingi ya kibinadamu ni muhimu katika migogoro yote ya kimataifa na lazima itekelezwe kwa usawa katika maeneo yote ya vita. Misaada ya kibinadamu haipaswi kamwe kuwa na matashi ya kisiasa, na ardhi ya Palestina haipaswi kupungua au kufanyiwa mabadiliko ya idadi ya watu.

Israel imezuia kuingia vifaa vya matibabu, chakula na mafuta Ghaza tangu mwanzoni mwa mwezi Machi mwaka huu wakati ilipoanzisha wimbi jipya la jinai zake na baada ya kukanyaga makubaliano ya kusimamisha vita kati yake na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, HAMAS.

Jinai za utawala wa Kizayuni ni kubwa mno na hazivumiliki kiasi kwamba hata viongozi wa Uingereza, Canada na Ufaransa wametishia kuiwekea vikwazo Israel kutokana na uhalifu wa kivita na jinai za kutisha huko Ghaza. Tishio hilo limezidisha mashinikizo kwa nduli wa Ghaza, yaani waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.