Maiti 58 wapatikana katika hospitali ya Libya ya wanamgambo wa SSA
(last modified Tue, 20 May 2025 06:50:15 GMT )
May 20, 2025 06:50 UTC
  • Maiti 58 wapatikana katika hospitali ya Libya ya wanamgambo wa SSA

Takriban miili 58 ya watu ambao hawajulikani, ilipatikana jana Jumatatu katika hospitali moja mjini Tripoli iliyokuwa inadhibitiwa na wanamgambo wa SSA ambao kiongozi wao aliuawa wiki iliyopita.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Libya imetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, maiti hao wamepatikana kwenye jokofu la kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Abu Salim kwenye kitongoji chenye watu wengi cha Abu Salim, kusini mwa Tripoli, mji mkuu wa Libya.

Wanamgambo wa SSA hawakuripoti kuwepo maiti hao. Picha za maiti walio na nambari na nyuso zilizokaguliwa zimetumwa na wizara hiyo, zikionyesha miili hiyo ikiwa imeoza. Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Libya, miili ya maiti hao ilitelekezwa. Uchunguzi umeanza mara moja kubaini wasifu na utambulisho wa marehemu hao.

“Hadi sasa miili 23 imefanyiwa uchunguzi na taratibu zote muhimu za kisheria zimechukuliwa ikiwa ni pamoja na kuweka kumbukumbu na kukusanya sampuli,” imesema wizara hiyo.

Abu Salim ni kitongoji cha kusini mwa Tripoli huko Libya ambacho kilikuwa ni makazi ya wanamgambo wanaojulikana kwa jina la "Stabilization Support Apparatus (SSA)", ambao kiongozi wao, Abdulghani Kikli, aliyejulikana kwa jina maarufu la Ghaniwa, aliuawa katika mazingira ya kutatanisha Jumatatu ya wiki iliyopita.

Mauaji ya Kikli yamepelekea kushindwa ghafla wanamgambo wa SSA na vikundi vilivyoungana na Waziri Mkuu anayetambuliwa kimataifa Abdulhamid al-Dbeibah wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU).

Jumanne iliyopita, Dbeibah aliamuru makundi yenye silaha kusambaratishwa, na kusababisha mapigano makali zaidi kuwahi kutokea mjini Tripoli kati ya makundi mawili yenye silaha. Umoja wa Mataifa umesema kuwa, mapigano hayo yamesababisha vifo vya takriban raia wanane.