Iran, Misri zataka kukomeshwa mashambulizi ya Israel huko Gaza
(last modified Wed, 14 May 2025 02:46:37 GMT )
May 14, 2025 02:46 UTC
  • Iran, Misri zataka kukomeshwa mashambulizi ya Israel huko Gaza

Wanadiplomasia wakuu wa Iran na Misri wamesisitiza kuwa kuna haja ya kukomeshwa mashambulizi ya utawla wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, katika mazungumzo ya simu na mwenzake wa Misri Badr Abdul Ati, wamejadili maendeleo ya kikanda na mazungumzo ya nyuklia yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani.

Araghchi amemtaarifu mwenzake wa Misri kuhusiana na duru ya nne ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na Marekani mjini Muscat.

Abdul Ati, kwa upande wake, amethibitisha uungaji mkono wa Cairo kwa mazungumzo ya nyuklia na kumweleza Araghchi kuhusu juhudi za Misri na zile za wapatanishi wengine za kutaka kuhuishwa mapatano ya Gaza.

Aidha amesema anatumai kuwa mazungumzo kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Marekani yatapunguza mivutano katika eneo la Magharibi mwa Asia.

Pande hizo mbili zimesisitiza juu ya ulazima wa kukomeshwa mara moja hujuma za utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Gaza na uchokozo na uvamizi wa Israel dhidi ya Lebanon na Syria.

Kadhalika wanadiplomasia hao wakuu wa Iran na Misri wamesisitizia haja ya kuimarishwa uhusiano wa pande mbili kati ya Tehran na Cairo katika nyuga mbali mbali.