Wanajeshi, raia 28 wauawa katika hujuma za kigaidi Burkina Faso
Kwa akali watu 28 wakiwemo wanajeshi na raia wameuwa katika mashambulizi mawili ya kigaidi kaskazini mwa Burkina Faso.
Jeshi la nchi hiyo limesema kambi ya kijeshi ya Falagountou kaskazini mwa nchi hiyo karibu na mpaka wa Niger ilishambuliwa na watu waliojizatiti kwa silaha, ambapo wanajeshi 10, wapiganaji wawili wa kujitolea na raia mmoja wameuawa.
Taarifa ya jeshi hilo imeongeza kuwa, maiti 15 za wanamgambo waliotekeleza shambulizi hilo dhidi ya kambi ya kijeshi ya Falagountou zimepatikana pia katika eneo hilo.
Wakati huo huo, Gavana wa jimbo la Cascades, Jean Charles dit Yenapono amesema miili ya raia 15 imepatikana kusini mwa nchi karibu na mpaka wa Ivory Coast, kufuatia shambulio la Jumapili. Amesema maiti hizo zilipatikana jana Jumatatu katika kijiji cha Linguekoro zikiwa na athari za majeraha ya risasi.
Haya yanajiri wiki mbili baada ya watu tisa kuuawa wakati watu wanaoshukiwa kuwa magaidi wakufurishaji wenye misimamo ya kufurutu ada waliposhambulia msikiti mmoja katika kijiji cha Goulgountou katika eneo la Sahel, kaskazini mashariki mwa Burkina Faso.

Maelfu ya watu wameuawa na wengine zaidi ya milioni mbili wamekimbia makazi yao tangu magaidi hao wakufurishaji waanze kuishambulia Burkina Faso kutokea nchi jirani ya Mali mnamo 2015.
Hujuma na mashambulio ndani ya ardhi ya Burkina Faso yamechochea kuzuka mapinduzi mawili mwaka jana yaliyofanywa na maafisa wa jeshi waliokasirishwa na kuongezeka idadi ya raia wanaouawa katika mashambulio hayo.