Askari wa Kulinda amani wa UN auawa nchini DRC, Guterres alaani hujuma
(last modified Mon, 06 Feb 2023 07:41:23 GMT )
Feb 06, 2023 07:41 UTC
  • Askari wa Kulinda amani wa UN auawa nchini DRC, Guterres alaani hujuma

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amelaani vikali shambulio lililofanywa Jumapili huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC dhidi ya helikopta ya ujumbe wa umoja huo wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO, shambulio ambalo limesababisha kifo cha mlinda amani mmoja wa UN kutoka Afrika Kusini na mwingine kujeruhiwa.

Taarifa iliyotolewa Jumapili jijini New York, Marekani na msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric, imesema helikopta hiyo ya MONUSCO ilishambuliwa wakati ikiwa safarini kutoka mji wa Beni kuelekea Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, helikopta hiyo hatimaye iliweza kutua salama mjini Goma,

Hadi sasa hakuna taarifa zozote kuhusu mhusika wa shambuli hilo na aina ya kifaa kilichotumika kushambulia helikopta hiyo ikiwa angani.

 “Natoa salamu zangu za rambirambi kwa wananchi na serikali ya Afrika Kusini na nawatakia ahueni ya haraka majeruhi,” amenukuliwa Katibu Mkuu katika taarifa hiyo.

Guterres amerejelea kauli yake kwamba shambulizi dhidi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa linaweza kuwa uhalifu wa kimataifa kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

Ametoa wito kwa mamlaka za DRC zichunguze shambulio hilo la kikatili na wahusika wafikishwe haraka mbele ya sheria.

Hali kadhalika amesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa, kupitia Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu nchin ihumo utaendelea kusaidia serikali ya DRC na wananchi wake katika jitihada zao za kuleta amani mashariki mwa nchi hiyo.

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Afrika Kusini ni miongoni mwa walinda amani kutoka mataifa 10 wanaotekeleza jukumu la ulinzi wa amani mashariki mwa DRC ambako waasi wamekuwa wakifanya mashambulizi kwa miongo kadhaa sasa.

 

Tags