Lavrov: Tutaisadia Afrika Magharibi katika vita dhidi ya makundi yenye silaha
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i93828-lavrov_tutaisadia_afrika_magharibi_katika_vita_dhidi_ya_makundi_yenye_silaha
Sergei Lavrov Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ameahidi msaada wa nchi yake kwa nchi za Magharibi mwa Afrika katika kupambana na makundi yanayobeba silaha. Moscow imebainisha hayo katika juhudi za kupanua ushawishi wake barani Afrika wakati huu Russia ikiendelea kuvutana kidiplomasia na mataifa ya Magharibi.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Feb 09, 2023 02:19 UTC
  • Lavrov: Tutaisadia Afrika Magharibi katika vita dhidi ya makundi yenye silaha

Sergei Lavrov Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ameahidi msaada wa nchi yake kwa nchi za Magharibi mwa Afrika katika kupambana na makundi yanayobeba silaha. Moscow imebainisha hayo katika juhudi za kupanua ushawishi wake barani Afrika wakati huu Russia ikiendelea kuvutana kidiplomasia na mataifa ya Magharibi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amepongeza hatua ya kuasisiwa muungano kati ya Moscow na Bamako kwa lengo la kupambana na makundi yenye silaha. Ametoa pongezi hizo akiwa katika ziara yake ya kwanza huko Mali ambayo ameitaja kuwa ni ya kihistoria. 

Sergei Lavrov amewaambia waandishi wa habari mjini Bamako kuwa, mapambano dhidi ya ugaidi ni kadhia inayozihusu pia nchi nyingine za eneo la Magharibi mwa Afrika. "Tutaendelea kuzipatia msaada nchi za Magharibi mwa Afrika ili kuondokana na masaibu haya. Suala hili linazihusu Guinea, Burkina Faso, Chad na eneo la Sahel kwa ujumla", amesema Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia.  

Waasi wa Mali 

Nchi ya Mali kwa muda mrefu imekuwa ikitegemea usaidizi wa kijeshi kutoka Ufaransa, nchi mkoloni wa zamani wa nchi hiyo, ili kupambana dhidi ya makundi yanayobeba silaha. Hata hivyo Paris iliondoa wanajeshi wake huko Mali mwaka jana baada ya kupamba moto mivutano kati yake na serikali ya kijeshi Mali. 

Tangu itwae madaraka mwaka 2020, serikali ya kijeshi ya Mali imeingiza nchini humo ndege kutoka Russia, helikopta na wanamgambo ili kuimarisha mapambano yake dhidi ya waasi wanaobeba silaha.

Kwa upande wake Ufaransa inasema kuwa vikosi hivyo vya Russia vilivyoko Mali ni mamluki wa kampuni ya Wagner ambalo ni kundi binafsi linalojishusisha na masuala ya kijeshi, ambalo pia limetumwa hukoSyria na Ukraine.