UNHCR yaipongeza Tanzania kwa kuendelea kuwa kimbilio la waliofukuzwa makwao
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i93928-unhcr_yaipongeza_tanzania_kwa_kuendelea_kuwa_kimbilio_la_waliofukuzwa_makwao
Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR Filippo Grandi amepongeza utamaduni wa muda mrefu wa Tanzania wa kukaribisha wakimbizi, sambamba na juhudi za taifa hilo za kuendelea kukidhi mahitaji ya wale wanaokimbia ghasia makwao.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Feb 11, 2023 11:57 UTC
  • UNHCR yaipongeza Tanzania kwa kuendelea kuwa kimbilio la waliofukuzwa makwao

Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR Filippo Grandi amepongeza utamaduni wa muda mrefu wa Tanzania wa kukaribisha wakimbizi, sambamba na juhudi za taifa hilo za kuendelea kukidhi mahitaji ya wale wanaokimbia ghasia makwao.

Grandi ametoa pongeza hizo katika mazungumzo na Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania yaliyofanyika Dodoma, mji mkuu wa shughuli za serikali ambako Kamishna Mkuu huyo wa UNHCR alifika baada ya kuhitimisha ziara yake nchini Burundi.

Katika mazungumzo hayo, Samia na Grandi, wamejadili pamoja na mambo mengine, maendeleo katika kuweka mazingira mazuri kwa wakimbizi wa Burundi walioko nchini humo kurejea nyumbani.

"Timu zetu zitaendelea kushirikiana kwa karibu na serikali ya Burundi na Tanzania, wadau na wahisani wakiwemo wale wa maendeleo ili kulinda na kusaka majawabu ya wale waliokimbia makwao", amesema Grandi katika mazungumzo yake hayo na rais wa Tanzania.

Wakimbizi wa Burundi walioko Tanzania

Takribani wakimbizi 248,000 na wasaka hifadhi, wengi wao kutoka Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC wanaishi nchini Tanzania, taifa ambalo linaongoza duniani kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya wakimbizi kutoka Burundi.

Kabla ya hapo, mnamo Agosti 2022, Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi aliitembelea Tanzania ambapo aliwahimiza wahisani kuunga mkono zaidi suluhu na hiari juu ya suala la wakimbizi na kusifu maendeleo yaliyopigwa katika ulinzi wa wakimbizi nchini humo.

Katika ziara yake hiyo, Grandi alipongeza pia juhudi za serikali ya Tanzania za kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wakimbizi, akibainisha kuwa hatua hiyo itawapa ulinzi muhimu wa kisheria na kupunguza hatari ya kutokuwa na utaifa, huku pia ikitoa aina ya utambulisho wanaporejea katika nchi yao ya asili.../