Upinzani DRC: Usajili wa wapigakura umefanyika kwa maslahi ya muungano tawala
(last modified Tue, 21 Feb 2023 07:48:01 GMT )
Feb 21, 2023 07:48 UTC
  • Upinzani DRC: Usajili wa wapigakura umefanyika kwa maslahi ya muungano tawala

Vyama vya upinzani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo vimekosoa mchakato wa kusajili mapema wapiga kura nchini humo kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Disemba mwaka huu.

Vyama hivyo vya upinzani vimesema mchakato huo wa usajili wa wapigakura, mbali na kukumbwa na kasoro chungu nzima, lakini umefanyika pia kwa maslahi na kuupendelea muungano wa kisiasa unaotawala nchini humo.

Viongozi wa upinzani nchini DRC wametilia shaka mwenendo mzima wa kuwaandikisha wapiga kura katika madaftari ya kudumu ya wapigakura, wakisisitiza kuwa usajili huo umekumbwa na changamoto tele, na katika baadhi ya maeneo haujafanyika kwa uwazi.

Uandikishaji wa mapema wa wapiga kura nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ulianza mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka uliopita wa 2022.

Wananchi wa Kongo wasiopungua milioni 50 katika nchi hiyo yenye majimbo 26, wanatazamiwa kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura, zoezi ambalo limekumbwa na changamoto nyingi zikiwemo za kiufundi.

Rais Felix Tshisekedi anatazamia kuwania tena kiti cha urais huko Kongo baada ya kuhitimisha muhula wake wa kwanza wa urais uliogubikwa na matatizo ya kiuchumi na kuibuka kwa harakati za waasi mashariki mwa nchi hiyo.

Baadhi ya viongozi wa upinzani wanaotazamiwa kuchuana na Rais Tshisekedi katika uchaguzi huo ni pamoja na Martin Fayulu na Moise Katumbi, gavana wa zamani wa jimbo la Katanga mwenye ushawishi mkubwa katika siasa wa DRC. 

Zoezi hilo la kusajili wapiga kura nchini Kongo tangu mwanzoni liliripotiwa kusuasua kutokana na uhaba wa vifaa licha ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (CENI) kuzindua mfumo mpya wa usajili wa awali wa simu za rununu ili kuharakisha mchakato na kuzuia misururu mirefu iliyojitokeza wakati wa uchaguzi uliopita. Vipimo vya utambuzi wa macho (iris) pia vimetajwa kuongezwa ili kupunguza udanganyifu.

 

Tags