Ombi la Uganda kwa Algeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i9445-ombi_la_uganda_kwa_algeria
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda ameiomba Algeria iiunge mkono nchi hiyo katika kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Kamisheni ya Utekelezaji ya Umoja wa Afrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 18, 2016 06:50 UTC
  • Ombi la Uganda kwa Algeria

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda ameiomba Algeria iiunge mkono nchi hiyo katika kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Kamisheni ya Utekelezaji ya Umoja wa Afrika.

Henry Okello, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda amewasilisha ombi hilo katia mazungumzo aliyofanya na waziri mwenzake wa Algeria, Ramtane Lamamra huko Algiers. Okello amesisitiza umuhimu wa nafasi hiyo ambayo inahitajia weledi na ujuzi wa kutosha ili kuweza kuziwakilishi nchi za bara la Afrika.

Kikao kijacho cha wakuu wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) ambacho kimepangwa kufanyika tarehe 10 hadi 18 mwezi Julai huko Kigali mji mkuu wa Rwanda, kitachunguza na kujadili suala la kumchagua mrithi wa kiti cha bi Nkosazana Dlamini Zuma. Zuma ni mwaharakati wa kisiasa kutoka Afrika Kusini ambaye kwa sasa ndiye anayeshikilia nafasi ya Mwenyekiti wa Kamisheni ya Utendaji ya Umoja wa Afrika.

Kamisheni hiyo kama lilivyo na Baraza la Amani na Usalama, Bunge la Pan African na Baraza la Masuala ya Kiuchumi, Kitamaduni na Kijamii, ni miongoni mwa mihimili muhimu ya Umoja wa Afrika. Jukumu la taasisi hiyo ni kulinda mamlaka ya kitaifa na ardhi za nchi 54 wanachama wa umoja huo. Kutatuliwa kwa amani migogoro na kubainishwa nafasi ya bara la Afrika katika mahusiano ya kimataifa pia ni miongoni mwa kazi muhimu za taasisi hiyo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda amefanya safari huko Algeria ili kupata uungaji mkono wa nchi hiyo ambapo kwa sasa umesalia muda mchache hadi kufanyika kikao cha wakuu wa Umoja wa Afrika cha kuainisha Mwenyekiti Mpya wa Kamisheni ya Utekelezaji ya umoja huo. Uungaji mkono wa serikali ya Algeria kwa mgombea kutoka Uganda katika kinyang'anyiro cha kuchagua kiongozi wa nafasi ya juu ya uongozi ndani ya Umoja wa Afrika, utakuwa na mchango muhimu. Henry Okello Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda ambaye kitaaluma ni mwanasheria na wakati huohuo ni mwanasiasa, ndiye mgombea wa kiti hicho muhimu katika Umoja wa Afrika. Okello ambaye aliingia katika siasa za Uganda mwaka 2001, anatambulika kama shakhsia mkubwa katika medani ya uongozi nchini humo.

Okello alimshinda hasimu wake kutoka chama cha upinzani katika uchaguzi wa bunge uliofanyika mwezi Machi mwaka 2011 na hivyo kufanikiwa kuingia bungeni. Chama cha upinzani cha Uganda People's Congress (UPC) kiliutaja ushindi wa Henry Okello kuwa ulitokana na uungaji mkono wa chama tawala cha NRM.

Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanasema kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda anagombea nafasi hiyo ikiwa ni katika mwendelezo wa sera za kupenda jaha na madaraka za Rais Yoweri Museveni wa nchi hiyo. Museveni ambaye yuko madarakani Uganda tangu mwaka 1986, alishinda uchaguzi wa rais wa mwezi Februari mwaka huu na hivyo kuweza kulinda nafasi yake hiyo kwa mara ya tano. Rais Museveni pia anafanya jitihada ili kuidhihirisha Uganda kuwa ni nchi yenye nguvu kiuchumi na kisiasa kati ya nchi za eneo la katikati mwa Afrika kwa kukubali kuwa msuluhisi katika migogoro ya kieneo.