Umoja wa Mataifa watiwa wasiwasi na ongezeko la njaa nchini Sudan
Umoja wa Mataifa umeelezea wasiwasi wake kuhusu ongezeko la njaa na idadi ya wakimbizi nchini Sudan mwaka huu wa 2023.
Sudan ambayo iko Kaskazini Mashariki mwa Afrika, ni mojawapo ya nchi ambazo zinakabiliwa na tatizo kubwa la uhaba wa chakula.
Umoja wa Mataifa ulitangaza katika ripoti yake iliyochapishwa Jumapili kwamba watoto milioni 4 walio chini ya umri wa miaka mitano na wanawake wajawazito na akina mama wanaonyonyesha nchini Sudan wanahitaji huduma muhimu ili kuishi, na kusisitiza kwamba idadi ya watu wanaokabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula imeongezeka kwa mwaka wa tatu mfululizo.
Huku ukisisitiza kuwa ni watu milioni mbili pekee waliokabiliwa na tatizo la njaa nchini Sudan mwaka uliopita wa 2022, Umoja wa Mataifa umesema kuwa Sudan ni miongoni mwa nchi zilizo hatarini zaidi duniani, huku asilimia 13.6 ya raia wake wakikabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula.
Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa, uchumi wa Sudan unaendelea kudorora siku hadi siku tangu mapinduzi ya Oktoba 2021 na kusitishwa misaada ya kimataifa kwa nchi hiyo, na inatabiriwa kuwa takriban watu milioni 15.8 watahitajia misaada ya kibinadamu mwaka huu ambapo watu milioni 1.5 wameongezeka kwenye orodha ya mwaka uliopita.
Sudan ni mojawapo ya nchi zinazokabiliwa na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa. Mvua kubwa na mafuriko mwaka 2022 yaliathiri maisha ya watu wapatao laki 3.49 katika nchi hiyo ya Afrika, huku homa ya dengue na malaria pia ikisambaa kutokana na maji yaliyotuama nchini.
Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa, kiwango cha maambukizi ya malaria katika majimbo 14 kati ya 18 ya Sudan mwaka 2022 kilizidi kiwango kilichowekwa, ambacho ni mara mbili ya kile kilichoshuhudiwa mwaka 2021.