Waasi 8 wa ADF wauawa, 9 wakamatwa mashariki mwa DRC
(last modified Wed, 01 Mar 2023 07:07:31 GMT )
Mar 01, 2023 07:07 UTC
  • Waasi 8 wa ADF wauawa, 9 wakamatwa mashariki mwa DRC

Kwa akali wanamgambo wanane wa kundi la ADF wameuawa huku wengine tisa wakitiwa mbaroni katika operesheni ya jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika mkoa wa Kivu Kaskazini, mashariki mwa nchi.

Hayo yamesemwa na Luteni Kanali Mak Hazukay, msemaji wa vikosi vya pamoja vya DRC na Uganda katika mahojiano na shirika la habari la Anadolu na kuongeza kuwa, waasi hao wameuawa katika makabiliano makali ya Jumatatu katika kijiji cha Mwalika mjini Beni.

Amesema mbali na kuwatia mbaroni wanamgambo tisa, wanajeshi hao wa Kongo DR na Uganda wamefanikiwa kutwaa silaha mbalimbali yakiwemo mabomu, mkoba wa risasi na vifaa vya mawasiliano vilivyokuwa mikononi mwa waasi hao wa ADF.

Makabiliano hayo mapya yamejiri siku chache baada ya vikosi hivyo vya pamoja kushambulia ngome ya wanamgambo wa ADF katika Bonde la Mwalika, wakila njama za kushambulia vijiji vya Beni katika mkoa wa Kivu Kaskazini, mashariki mwa nchi.

Vikosi hivyo vya kieneo vimetoa mwito kwa magenge ya waasi na wanamgambo mashariki mwa Kongo DR kuweka silaha chini na kujisalimisha kwa vyombo husika vya usalama.

Ramani ya DRC inayoonesha mikoa mitatu ya mashariki inayosumbulia na ukosefu wa usalama

Hii ni katika hali ambayo, hivi karibuni Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (MONUSCO) kilitangaza habari ya kusimamisha ndege zake kuruka katika anga ya mkoa huo wa Kivu Kaskazini, baada ya helikopta yake kushambuliwa Ijumaa iliyopita.

Wanachama wa kundi la waasi la M23 na kundi la kigaidi la ADF wameendelea kuyumbisha usalama mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, licha ya uwepo wa askari wa UN, wanajeshi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na vikosi vya usalama vya DRC.

Tags