Mafuriko yahofiwa kuongeza hatari ya kipindupindu barani Afrika
Shirika la Afya Duniani WHO limetahadharisha kuwa, ingawa idadi ya wagonjwa wa kipindupindu ya kila wiki katika nchi zilizoathirika na mripuko wa ugonjwa huo barani Afrika inapungua, lakini mafuriko makubwa yanayotokana na mvua za msimu na vimbunga vya kitropiki kusini mwa Afrika yanaongeza hatari ya ugonjwa huo kuenea na kutishia kudhoofisha juhudi za kuudhibiti.
Takwimu za WHO zinaonyesha kwamba idadi ya wagonjwa wapya wa kipindupindu ilipungua hadi 2,880 katika wiki iliyomalizika tarehe 26 Februari, ikiwa ni punguo la asilimia 37 ikilinganishwa na wiki kabla ya hiyo ambapo idadi ya wagonjwa iliyorekodiwa ilikuwa 4,584.
Pia idadi ya vifo haina mabadiliko makubwa ikipungua kidogo tu kutoka watu 82 hadi 81 katika kipindi hicho hicho.
Nchi 12 za Afrika zinaripoti wagonjwa wapya wa kipindupindu ikiwa ni pamoja na Afrika Kusini, Tanzania na Zimbabwe.

Kwa upande wa eneo la kusini mwa Afrika, Shirika la Afya Duniani limesema miripuko hiyo ya kipindupindu inakuja huku kukiwa na mvua za msimu na dhoruba za kitropiki ambazo zimesababisha mafuriko makubwa.
WHO imetolea mfano Malawi, ambayo inakabiliwa na mripuko mbaya zaidi wa kipindupindu katika historia yake, na kutahadharisha kuwa kuongezeka kwa mvua kunapunguza juhudi za kudhibiti mripuko katika baadhi ya maeneo.
Kwa mujibu wa ripoti ya shirika hilo la UN, timu za kukabiliana na hali hiyo zinapata changamoto kubwa kuwafikia watu wanaohitaji huduma kutokana na ugumu wa barabara na miundombinu iliyoharibika.
Ili kusaidia vita dhidi ya kipindupindu katika ukanda wa kusini mwa bara la Afrika, WHO imetuma wataalam 80 katika nchi zilizoathirika.
Katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, shirika hilo la afya duniani limesafirisha tani 455 za vifaa muhimu vya kukabiliana na kipindupindu kuelekea Malawi na Msumbiji.
Vifaa hivyo vimepelekwa pia Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC, Ghana, Kenya na Zambia ili kuimarisha maandalizi na kukabiliana na janga hilo la kipindupindu.../