Sudan kususia sarafu ya dola ya Marekani katika biashara na Russia
(last modified Sun, 12 Mar 2023 11:33:10 GMT )
Mar 12, 2023 11:33 UTC
  • Sudan kususia sarafu ya dola ya Marekani katika biashara na Russia

Sudan inatafakari kusitisha matumizi ya sarafu ya dola ya Marekani katika miamala yake ya kibiashara na Russia.

Hayo yamesemwa na Hassan Mohammed Elghazali Eltijani Sirraj, Balozi wa Sudan nchini Russia katika mahojiano na shirika la habari la RIA Novosti na kuongeza kuwa, Khartoum ina hamu ya kuimarisha biashara na Russia.

Kwa mujibu wa mwanadiplomasia huyo, Benki Kuu za nchi mbili hizo zinajadiliana hivi sasa kuhusu suala hilo la kuweka pembeni sarafu ya dola ya Marekani katika miamala yao, na badala yake zitumie fedha za ndani za nchi hizo kwenye mabadilishano hayo.

Nchi nyingi duniani hivi sasa zipo mbioni kusitisha matumizi ya dola za Marekani. Februari mwaka huu, serikali ya Sudan Kusini, ilitangaza kusitisha matumizi ya dola ya Marekani na badala yake ikaagiza shughuli zote zifanyike kwa fedha za ndani, yaani Pauni ya Sudan Kusini (SSP).

Aidha Novemba mwaka jana pia, serikali ya Ghana iliandaa sera mpya ya kununua bidhaa za mafuta kwa kutumia dhahabu badala ya sarafu ya dola ya Marekani.

Kadhalika kwa miezi kadhaa sasa, Russia imezipiga na chini na kuziweka pembeni sarafu za dola na euro katika miamala yake ya kimataifa, utokana na vikwazo vya nchi za Magharibi vilivyoshtadi baada ya kuanza vita vya Ukraine Februari mwaka uliopita.

Miaka kadhaa iliyopita, Uturuki na Russia zilitia saini mapatano ya kutupilia mbali sarafu ya dola katika mabadilishano ya kibiashara baina yao, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa nchi hizo mbili kuacha kutegemea sarafu hiyo ya Marekani.

Tags