Ripoti: Ukame uliua watu zaidi ya 40,000 nchini Somalia 2022
Utafiti uliofanywa na Wizara ya Afya ya Uswisi, Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) umeonyesha kuwa, ukame ambao ni mrefu zaidi kuwahi kurekodiwa nchini Somalia umesababisha makumi ya maelfu ya watu kupoteza maisha.
Matokeo ya utafiti huo yanasema kuwa, zaidi ya watu 43,000 yumkini waliaga dunia kutokana na janga la ukame lililoikumba nchi hiyo ya Pembe ya Afrika mwaka 2022.
Utafiti huo wa pamoja na Wizara ya Afya ya Uswisi, WHO na UNESCO umebainisha kuwa, nusu ya vifo hivyo vilivyosajiliwa mwaka jana kutokana na ukame nchini Somalia vilikuwa miongoni mwa watoto waliokuwa na umri wa chini ya miaka mitano.
Akizungumzia utafiti huo, Ali Hadji Adam Abubakar, Waziri wa Afya wa Somalia ameiasa jamii ya kimataifa kuchukua hatua za kuipiga jeki sekta ya afya ya nchi hiyo ambayo pia inakabiliwa na mapigano na mashambulizi ya genge la kigaidi la al-Shabaab.
Mwenendo huo wa ukame nchini Somalia na katika maeneo mengine ya Pembe ya Afrika unaripotiwa kuwa mbaya zaidi hivi sasa kuliko ilivyokuwa wakati wa njaa ya mwaka 2011, ambapo mamia ya maelfu ya watu waliaga dunia.
Hivi karibuni, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia alitahadharisha kuwa, vifo zaidi vitarekodiwa nchini humo na vitapindukia idadi ya watu waliopoteza maisha wakati njaa ilipoiathiri nchi hiyo mwaka 2011; ambapo watu zaidi ya 260,000 waliaga dunia kwa kukosa chakula.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, Somalia hivi sasa inakabiliwa na misimu mitano mfululizo ya kutonyesha mvua, jambo ambalo linawafanya Wasomalia milioni tano kukabiliwa na ukosefu wa usalama wa chakula, huku watoto milioni mbili wakikodolewa macho na utapiamlo.