Waasi wa CODECO waua mateka 17 mashariki mwa Kongo
(last modified Mon, 27 Mar 2023 08:03:32 GMT )
Mar 27, 2023 08:03 UTC
  • Waasi wa CODECO waua mateka 17 mashariki mwa Kongo

Wanamgambo wenye sifa mbaya huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo jana waliwaua watu 17 ambao waliwateka nyara siku moja kabla ya kutekeleza mauaji hayo.

Banguneni Gbalande kiongozi wa kijamii katika jimbo la Ituri ameeleza kuwa waasi wa CODECO wamewaua watu 17 ambao waliwateka nyara juzi katika eneo la Djugu umbali wa kilomita 45 kaskazini mwa jimbo la Bunia. Mkuu mwingine wa kikabila kwa jina la Toko Kaqbanese amesema kuwa mateka wote wameuliwa na wanamgambo wa CODECO.  

CODECO, Jumuiya ya Ushirika wa Maendeleo ya Kongo, ni moja ya maelfu ya makundi yenye silaha yanayoendesha harakati zao katika jimbo  lililokumbwa na machafuko na lenye utajiri wa madini la Ituri.

Watu hao 17 waliouawa walitekwa nyara na waasi wa CODECO juzi Jumamosi baada ya wanachama watatu wa harakti hiyo kuuawa katika majibizano na kundi jingine hasimu huko Bambu. Mama mjamzito ni kati ya raia waliokuwa wametekwa nyara na waasi wa CODECO juzi Jumamosi. 

Ripoti zinasema kuwa tokea mwaka jana wa 2022 kila wiki makumi ya watu wamekuwa wakiuliwa katika jimbo la Ituri lenye utajiri wa madini ya dhahabu.

 

Tags