Watu 14 waaga dunia baada ya mgodi kuporomoka Sudan
(last modified Sat, 01 Apr 2023 09:21:55 GMT )
Apr 01, 2023 09:21 UTC
  • Watu 14 waaga dunia baada ya mgodi kuporomoka Sudan

Kwa akali watu 14 wamefariki dunia baada ya kuporomokewa na udongo kwenye mgodi wa dhahabu wa Jebel Al-Ahmar katika jimbo la Kaskazini nchini Sudan, mpakani na Misri.

Afisa wa ngazi ya juu wa Shirika la Rasilimali za Madini la Sudan aliliambia shirika la habari la Reuters jana Ijumaa kuwa, mbali na wachimba migodi14 kuaga dunia kwenye ajali hiyo, wengine zaidi ya 20 wamejeruhiwa na wanatibiwa katika hospitali iliyoko karibu na eneo la tukio.

Msemaji wa shirika hilo la serikali, Moataz Hajj amesema majeruhi walinusuriwa katika operesheni ya uokoaji, na kwamba walioaga dunia wameshahimiwa katika mji wa Wadi Halfa na tayari wameshazikwa.

Mashuhuda wamenukuliwa na shirika rasmi la habari la Sudan SUNA wakisema kuwa, wachimba migodi hao waliporomokewa na udongo kwa kuwa walikuwa wanatumia mitambo mizito kwenye timbo hilo wakisaka dhahabu.

Ikumbukwe kuwa, Disemba mwaka 2021, watu 38 walipoteza maisha baada ya kuporomokewa na mgodi wa dhahabu wa Darsay katika kijiji cha Fuja, mkoani Kordofan Magharibi, katikati mwa Sudan.

Dhahabu

Sudan ni moja ya nchi za bara Afrika zenye utajiri mkubwa wa madini hususan dhahabu, ingawaje shughuli za uchimbaji madini katika aghalabu ya matimbo ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika zinafanyika kinyume cha sheria na bila ya uangalizi wa vyombo vya dola.

Mwaka 2020, Sudan ilizalisha tani 36.6 za dhahabu, ikiwa ni nchi ya pili barani Afrika kuzalisha kiwango kikubwa zaidi cha madini hayo yenye thamani ndani ya mwaka mmoja.

Tags