Poda za Kimarekani za Johnson & Johnson zinasababisha saratani, Tanzania yaanzisha uchunguzi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i96040-poda_za_kimarekani_za_johnson_johnson_zinasababisha_saratani_tanzania_yaanzisha_uchunguzi
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) linachunguza uwezekano wa kuwepo kwenye soko poda za watoto zinazotengenezwa na kampuni kubwa ya dawa ya Marekani, Johnson & Johnson (J&J), ambazo imebainika kuwa zinasababisha saratani.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 08, 2023 11:28 UTC
  • Poda za Kimarekani za Johnson & Johnson zinasababisha saratani, Tanzania yaanzisha uchunguzi

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) linachunguza uwezekano wa kuwepo kwenye soko poda za watoto zinazotengenezwa na kampuni kubwa ya dawa ya Marekani, Johnson & Johnson (J&J), ambazo imebainika kuwa zinasababisha saratani.

Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Athuman Ngenya amesema shirika hilo limeanza kukusanya sampuli za poda za J&J kwa ajili ya uchunguzi mpya wa kimaabara.

"Baada ya kupata taarifa hizi, tulianza uchunguzi ili kubaini iwapo poda zinazozungumziwa zimeingia nchini ili tuchukue hatua stahiki," amesema Ngenya.

Haya yanajiri baada ya J&J Jumanne iliyyopita kupendekeza kutoa Dola za Kimarekani bilioni 8.9 ili kutatua kesi za miaka mingi zinazodai kuwa bidhaa zake za poda zimesababisha maradhi ya saratani.

Katika taarifa, kundi la mawakili ambao wanawakilisha karibu walalamikaji 70,000 nchini Marekani, ikiwa ni pamoja na familia za watu waliokufa kutokana na saratani ya ovari na mesothelioma, wameelezea mpango huo kama ushindi mkubwa kwa makumi ya maelfu ya wanawake wanaosumbuliwa na saratani ya uzazi inayosababishwa na bidhaa za J.&J.

Uchunguzi: Poda za Johnson Johnson zinasababisha saratani

Mnamo 2020, kampuni hiyo ilisema itasitisha uuzaji wa poda yake ya watoto zenye mada ya talc nchini Marekani na Canada. Kampuni hiyo imesema inapanga kuacha kuuza bidhaa hiyo duniani kote mwaka huu.

Makampuni ya Marekani yana historia mbaya ya kujaribu au kuuza dawa na bidhaa zenye madhara kwa binadamu hususan katika nchi zinazoendelea. Kwa mfano kampuni ya Kimarekani ya Pfizer ilifanya majaribio ya dawa mpya ya antibiotiki, Trovan katika jimbo la Kano kaskazini mwa Nigeria mwaka 1996.

Mgogoro wa kisheria wa muda mrefu uliibuka na hatimaye kampuni hiyo kubwa ya kutengeneza dawa ikalazimika kuwalipa fidia wazazi ambao watoto wao walishirikishwa katika majaribio ya dawa hiyyo wakati wa mlipuko wa ugonjwa wa utindio wa ubongo. Watoto 11 walifariki dunia na makumi ya wangine kupooza baada ya kupewa dawa ya kuzuia maumivu iliyokuwa ikifanyiwa majaribio na shirika hilo la Kimarekani.