Miaka tisa baada ya utekaji Chibok, UNICEF yataka wanafunzi walindwe Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i96274-miaka_tisa_baada_ya_utekaji_chibok_unicef_yataka_wanafunzi_walindwe_nigeria
Ikiwa imepiita miaka tisa tangu wasichana 276 watekwe nyara wakiwa katika shule ya bweni huko Chibok, Nigeria, ambapo mpaka sasa 96 bado wapo utumwani, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limetaka wadau kusaidia katika kuwekeza zaidi katika usalama wa wanafunzi mashuleni kwani bado vitendo vya utekaji nyara vinaendelea nchini humo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 15, 2023 02:10 UTC
  • Miaka tisa baada ya utekaji Chibok, UNICEF yataka wanafunzi walindwe Nigeria

Ikiwa imepiita miaka tisa tangu wasichana 276 watekwe nyara wakiwa katika shule ya bweni huko Chibok, Nigeria, ambapo mpaka sasa 96 bado wapo utumwani, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limetaka wadau kusaidia katika kuwekeza zaidi katika usalama wa wanafunzi mashuleni kwani bado vitendo vya utekaji nyara vinaendelea nchini humo.

Mwakilishi wa UNICEF nchini Nigeria, Cristian Munduate, amesema vitendo vya utekaji nyara wanafunzi Kaskazini Mashariki mwa Nigeria vimefurutu ada ambapo taarifa za hivi karibuni za vyombo vya habari zinasema wanafunzi 80 wametekwa nyara na wanamgambo katika eneo la Tsafe jimboni Zamfara.

Muduate amesema: “Hatuwezi kufumbia macho mateso ya watoto wa Nigeria. Lazima tufanye kila tunachoweza kuhakikisha watoto hawa wanakuwa katika mazingira salama, wanapata elimu na fursa nyingine kadri ya uwezo wao.”

Tangu mwaka 2014 zaidi ya wanafunzi 6800 wameathirika. Lakini si wanafunzi pekee, kwani tangu mwaka 2009 takriban walimu 2300 wameuawa, 1900 hawajulikani walipo na shule 1500 zimefungwa kutokana na kukosekana usalama nchini Nigeria.

Akieleza zaidi changamoto wanazokutana nazo wanafunzi na walimu nchini humo, mwakilishi huyo wa UNICEF huko Nigeria ameeleza kuwa “takwimu zinaogofya, ikiwa imepita miaka 9 tangu utekaji nyara wa kutisha wa wasichana wa Chibok, jinamizi hilo linaendelea kwani watoto bado wanatekwa, wanasajiliwa kwa nguvu kupigana vitani, kuuawa, kujeruhiwa na wanaharibiwa maisha yao ya baadae.”

UNICEF imekaribisha ahadi ya serikali ya Nigeria ya kutenga dola milioni 314.5 ambazo zitaelekezwa katika usalama kwenye shule. UNICEF imesema itashirikiana na serikali kwenye kutekekeza mpango wa shule salama na kuhakikisha watoto wote waliotekwa na wanamgambo wanarejeshwa salama kuungana na familia zao.

UNICEF pia imezitaka pande zote kwenye mzozo nchini humo kuheshimu sheria za kimataifa, haki za binadamu na kulinda haki na ustawi wa watoto.