Madaktari Sudan: Zaidi ya watu 50 wameuawa, karibu 600 wamejeruhiwa katika mapigano
(last modified Sun, 16 Apr 2023 07:01:53 GMT )
Apr 16, 2023 07:01 UTC
  • Madaktari Sudan: Zaidi ya watu 50 wameuawa, karibu 600 wamejeruhiwa katika mapigano

Kamati Kuu ya Madaktari wa Sudan imetangaza kuwa takriban watu 56 wameuawa na wengine 595 wamejeruhiwa katika mapigano yanayoendelea nchini humo kati ya Jeshi na Kikosi cha Radiamali ya Haraka (RSF).

Kamati hiyo imesema imerekodi idadi ya vifo katika uwanja wa ndege wa Khartoum na Omdurman, pamoja na magharibi mwa Khartoum katika miji ya Nyala, El Obeid na El Fasher.

Mapigano na machafuko yanayoendelea nchini Sudan yamezusha wasiwasi mkubwa, huku nchi nyingi pamoja na taasisi muhimu za kimataifa ukiwemo Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika zikitoa wito kwa pande zinazopingana kujizuia na kufanya mazungumzo ili kumaliza uhasama uliopo.

Kupitia ujumbe wa twitter uliotumwa na msemaji wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa mwito wa kukomeshwa machafuko mara moja nchini Sudan.

Miito ya kukomeshwa vita na mapigano nchini Sudan inatolewa katika hali ambayo vikosi vya jeshi vimetupilia mbali uwezekano wowote wa kufanya majadiliano au mazungumzo na kikosi chenye nguvu cha kijeshi cha Radiamali ya Haraka (RSF), huku mapigano kati ya pande hizo mbili yakiwa yangali yanaendelea.

Katibu Mkuu wa UN, Antonio Guterres

Vikosi vya majeshi ya Sudan vimeeleza katika taarifa kupitia ukurasa wake wa Facebook ya kwamba: hakutakuwa na "majadiliano au mazungumzo hadi kitakapovunjwa kwanza kikosi cha RSF".

Kauli hiyo imetolewa baada ya RSF kudai kwamba wapiganaji wake wameteka maeneo kadhaa muhimu, ikiwa ni pamoja na ikulu ya rais, makazi ya mkuu wa jeshi, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Khartoum.

Hata hivyo Jeshi la Sudan limekanusha madai yote yaliyotolewa na Kikosi cha Radiamali ya Haraka.

Viongozi wa vikosi vya jeshi na wa RSF, ambao walikuwa washirika katika mapinduzi ya kijeshi ya 2021, wametupiana lawama za kuanzisha mapigano yaliyozuka jana Jumamosi huku kila upande ukitoa taarifa kinzani kuhusu nani kati yao anayeshikilia vituo na taasisi kuu za nchi.../

Tags