Umoja wa Afrika wakutana kuijadili Sudan;idadi ya vifo yakaribia 100
(last modified Mon, 17 Apr 2023 06:30:54 GMT )
Apr 17, 2023 06:30 UTC
  • Umoja wa Afrika wakutana kuijadili Sudan;idadi ya vifo yakaribia 100

Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika liliitisha kikao cha dharura jana kujadiliana hali ya kisiasa na usalama nchini Sudan.

Jeshi la Sudan na kikosi maalumu cha radiamali ya haraka (Rapid Support Forces), wameendelea kwa siku ya tatu kupambania  udhibiti wa taifa hilo, hali inayoashiria kutokuwa tayari kumaliza uhasama licha ya kuongezeka kwa mashinikizo ya kidiplomasia ya kieneo na kimataifa ya kusitisha mapigano.

Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika liliitisha kikao cha dharura jana kujadiliana hali ya kisiasa na usalama nchini Sudan, imesema taarifa fupi kupitia ukurasa wa Twitter.

Mapigano makali yanaendelea katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum, baada ya vita kuingia siku yake ya tatu, waliouawa wakikaribia 100 huku zaidi ya elfu moja wakijeruhiwa, kulingana na Shirika la Afya Duniani.

Kiongozi mkuu, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan (kushoto), na naibu kiongozi wa kijeshi wa Sudan, Mohamed Hamdan Dagalo.

 

Wasudani wengi wamejifungia majumbani mwao huku kukiwa na hofu ya mzozo wa muda mrefu ambao unaweza kuzidisha hali ya machafuko na kuvuruga matumaini ya kurejea kwenye demokrasia ya utawala wa kiraia.

Kumetolewa ripoti zinazokinzana kuhusu udhibiti wa Ikulu ya Rais katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum, katika siku ya tatu ya mapigano yanayoendelea kati ya jeshi na Vikosi vya Radiamali ya Haraka.

Mapigano hayo yalizuka baada ya mvutano kuhusu pendekezo la kuanzishwa utawala wa kiraia na kuunganishwa vikosi vyote ndani ya jeshi moja la taifa.

Mapigano ya sasa nchini Sudan ni kati ya vitengo vya jeshi vinavyomtii kiongozi mkuu, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, na vikosi vya RSF, vinavyoongozwa na naibu kiongozi wa kijeshi wa Sudan, Mohamed Hamdan Dagalo.

Tags