Mapigano yameanza tena katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum
Apr 19, 2023 07:00 UTC
Ripoti za vyombo vya habari zinaeleza kuwa mapigano yamezuka upya kati ya vikosi vya jeshi la Sudan vinavyoongozwa na Jenerali Abdel-Fattah al-Barhan na vikosi vya Radiamali ya Haraka RSF vinavyoongozwa na Mohammed Hamdan Daghlo maarufu kama Hamidati katika mji mkuu wa nchi hiyo Khartoum.
Chaneli ya televisheni ya Al-Jazeera imetangaza mapema leo kuwa mapigano kati ya vikosi vya jeshi na vikosi vya RSF yameanza tena katika mji mkuu Khartoum.
Kwa mujibu wa televisheni hiyo mapigano makali hivi sasa yanaendelea kati ya vikosi vya pande hizi mbili karibu na ikulu ya rais na makao makuu ya jeshi mjini humo.
Ripoti zingine zinasema milio ya miripuko imesikika karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Khartoum.
Mapema kabla ya hapo, jeshi la Sudan lilivishutumu vikosi vya Radiamali ya Haraka kwa kukiuka usitishaji mapigano wa masaa 24 kwa ajili ya masuala ya kibinadamu ambao ulianzishwa kwa upatanishi wa kimataifa na kuanza kutekelezwa saa 12 jioni ya jana.
Muungano wa Madaktari wa Sudan umetangaza kuwa hospitali 39 za Khartoum na mikoa jirani ya maeneo yenye mapigano haziwezi kutoa huduma, na hospitali tisa kati ya hizo zimeshambuliwa kwa makombora.
Kwa mujibu wa muungano huo, hospitali 16 pia zimelazimika kuhamisha utoaji huduma.
Asasi hiyo imeripoti pia kuwa idadi ya vifo vya raia vilivyosababishwa na mapigano hayo ni watu 144 na idadi ya majeruhi wa kijeshi na raia ni 1,409.
Hata hivyo Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani Tedros Adhanom ametangaza kuwa idadi ya waliofariki imefikia 270 na waliojeruhiwa wamefikia 2,600.
Wizara ya Afya ya Sudan imesisitiza kusitishwa mapigano na ufyatuaji risasi ambao umelenga pia sekta za afya mjini Khartoum na kutangaza kuwa vitengo vya afya na hospitali za binafsi na za umma vinakaribia kusambaratika kikamilifu na hali itakuwa mbaya zaidi ikiwa vita vitaendelea.../