DRC inataka kutumia mfumo wa malipo wa Russia badala ya Mastercard
(last modified Thu, 27 Apr 2023 10:50:36 GMT )
Apr 27, 2023 10:50 UTC
  • DRC inataka kutumia mfumo wa malipo wa Russia badala ya Mastercard

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) inatafakari kuanza kutumia mfumo wa malipo wa kadi ya Mir ya Russia badala za kadi za Kimagharibi za Visa na MasterCard. Hayo yamesemwa na Muhindo Nzangi Butondo Waziri wa Elimu ya Juu na Vyuo Vikuu wa DRC, katika mahojiano na Sputnik.

Amesema hatua hiyo itachukuliwa kutatua matatizo ya wanafunzi Wakongamani ambao ni miongoni mwa wanafunzi wa kigeni katika vyuo vikuu vya Russia wanaopata matatizo ya kulipa karo kutokana na vikwazo vinavyoongozwa na Marekani vya Magharibi dhidi ya benki za Russia. Vikwazo hivyo viliwekwa dhidi ya Russia kutokana na oparesheni zake za kijeshi nchini Ukraine. Hivi sasa walio na kadi za benki zilizounganishwa na mifumo wa Kimagharibi ya Visa na MasterCard hawewezi kuzitumia nchini Russia.

Waziri Nzangi Butondo amesema kuwa serikali ya Kongo inafahamu tatizo ambalo wanafunzi wa Kongo wanakabiliana nalo katika kupokea elimu ya juu nchini Russia na ameongeza kuwa DRC "inataka kujaribu" mfumo mpya wa malipo ulioanzishwa na Russia wa Mir.

Afisa huyo aliongeza kuwa DRC pia ina nia ya kukuza ujifunzaji wa lugha ya Kirusi miongoni mwa vijana wa Kongo, kwani mabadilishano kati ya nchi hizo mbili yanatarajiwa kuimarika katika miaka ijayo.

Amesema anaamini kwamba kujifunza Kirusi kutakuwa na manufaa kwa wanafunzi wa Kongo ili kukidhi kikamilifu mahitaji na mahitaji yao ya elimu, au kushirikiana na wawekezaji wa Kirusi nchini DRC.

Alidokeza kuwa maeneo ya ushirikiano kati ya vyuo vikuu vya Kongo na Russia yanalenga zaidi uhandisi wa umma, amani, usalama, uhandisi wa kompyuta, na usalama wa mtandao.

Hayo yanajiri wakati ambao, Chuo Kikuu cha Urafiki cha Watu wa Urusi (RUDN), ambacho kimetoa mafunzo kwa maelfu ya wanafunzi wa Kiafrika kwa miongo kadhaa, hivi karibuni kilirejesha jina lake la awali kwa heshima ya Patrice Lumumba, Waziri Mkuu wa kwanza wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Waziri Butondo amesema kuwa jina la Patrice Emery Lumumba linathaminiwa sana nchini Russia na ni ishara inayoimarisha urafiki kati ya Russia na Waafrika, hasa Wakongo.

 

Tags