Rais Kagame ziarani Tanzania, aeleza umuhimu wa nchi hiyo kwa Rwanda
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i96744-rais_kagame_ziarani_tanzania_aeleza_umuhimu_wa_nchi_hiyo_kwa_rwanda
Rais wa Rwanda, Paul Kagame, jana alianza ziara ya siku mbili nchini Tanzania inayolenga kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili huku akimpongeza mwenyeji wake, Rais Samia Suluhu Hassa kwa kufanya juhudi za kuupatia ufumbuzi mgogoro nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
(last modified 2025-10-16T03:06:03+00:00 )
Apr 28, 2023 02:23 UTC
  • Rais Kagame ziarani Tanzania, aeleza umuhimu wa nchi hiyo kwa Rwanda

Rais wa Rwanda, Paul Kagame, jana alianza ziara ya siku mbili nchini Tanzania inayolenga kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili huku akimpongeza mwenyeji wake, Rais Samia Suluhu Hassa kwa kufanya juhudi za kuupatia ufumbuzi mgogoro nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Rais Paul Kagame alikutana na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania kuhusu masuala mbalimbali yanayozihusu nchi mbili. Katika mazungumzo hayo Rais Kagame alisema kuwa Tanzania imechangia pakubwa katika kutafuta suluhu ya mgogoro huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongona na kwamba amani na utulivu ni hitajio lenye umuhimu mkubwa kwa ajili ya maendeleo na Umoja wa Afrika.   

Naye Rais Samia Suluhu Hassan alisema wanalenga kufufua uhusiano wa kibiashara baina nchi zao. "Kiwango cha biashara cha sasa ni kidogo hakiendani na raslimali tulizo nazo kwa nchi mbili,alisema Rais Samia." Amesema ziara ya Kagame nchini Tanzania imewapa muda mzuri wa kutathmini masuala yote ya ushirikiano baina ya nchi mbili na kubuni mbinu mpya za mashirikiano zaidi.  

Rais Samia Suluhu Hassan ameahidi kuimarisha bandari za Dar es Salaam na Tanga ili kutoa huduma kwa ufanisi kwa Rwanda.

Pande hizo mbili pia zimekikubaliana kuimarisha sekta za biashara, nishati, miundombinu, ulinzi na usalama. Ni vyema kuashiria hapa kuwa, Rwanda inategemea bandari ya Dar es salaam kupokea bidhaa mbalimbali kutoke nje.