Rais Tebboune: Kujiunga Algeria katika BRICS, sababu ya kustawi nchi hiyo
Rais wa Algeria amesema kuwa kujiunga nchi hiyo ya Kiafrika na kundi la BRICS kutaisaidia Algeria kupiga hatua.
Rais Abdel Majid Tebboune wa Algeria ameeleza haya katika mazungumzo na baadhi ya taasisi za vyombo vya habari nchini humo na kuongeza kuwa, kundi la BRICS linafadhili miradi mbalimbali huko Algeria; na kwamba Algeria na BRICS zitashirikiana pia katika upande wa kisiasa.
Rais Tebboune ameongeza kuwa, kundi la BRICS liimewekeza kiasi cha dola bilioni 100; kiwango ambacho ni zaidi ya mtaji wa Benki ya Dunia.
Nchi wanachama wa kundi la BRICS ni Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini. Nchi hizo kwa pamoja zinaunda zaidi ya asilimia 40 ya jamii nzima ya dunia huku zikidhibiti karibu robo ya uzalishaji wa ndani kimataifa.

Wakati huo huo, ripoti mpya ya Benki ya Dunia ya mwezi Aprili mwaka huu ilieleza kuwa nchi wanachama wa kundi la BRICS zimezitumulia kivumbi nchi za kundi la G-7 katika kiwango cha ushiriki kwenye ukuaji uchumi duniani.
Benki ya Dunia ilitangaza katika ripoti yake mpya kuwa, kiwango cha ukuaji wa uchumi wa nchi wanachama wa kundi la BRICS ambazo ni Russia, China, India, Brazil na Afrika Kusini mwaka 2023 kimefikia asilimia 32.1. Ripoti hiyo imesema ukuaji huo wa kiuchumi umepita ule wa nchi wanachama wa kundi la G-7 linaloundwa na Ujerumani, Ufaransa, Italia, Japan, Uingereza, Canada na Marekani.
Ripoti mpya ya Benki ya Dunia iliongeza kuwa, kiwango cha ushiriki wa nchi wanachama wa kundi la BRICS katika ukuaji uchumi duniani mwaka 2028 kitafikia aslimia 33.3 kwa mujibu wa makadirio yaliyofanywa.