Mchungaji Paul Mackenzie na wenzake kubakia rumande kwa siku 30 Kenya
-
Mhubiri tata wa Kikristo Paul Mackenzie
Mhubiri tata wa Kikristo Paul Mackenzie anayekabiliwa na tuhuma za kuwashawishi wafuasi wake wafunga ili wawe wa kwanza kwenda mbinguni na kukutana na Yesu, Paul Mackenzie na mkewe Rhoda Maweu pamoja na washukiwa wengine 16 watazuiliwa kwa siku 30 gerezani.
Hakimu mwandamizi wa mahakama ya Shanzu huko Mombasa, Yusuf Shikanda ametoa uamuzi huo kwa ombi la maafisa usalama waliotaka washukiwa hao 18 wazuiliwe kwa siku 90. Amesema suala la Shakahola, ambako shughuli ya ufukuaji makaburi kuondoa miili inaendelea, haliwezi likapuuzwa.
Hakimu Yusuf Shikanda amesema: “Pia usalama wa washukiwa hauwezi ukapuuzwa. Wanaweza wakadhuriwa endapo wataachiliwa kwa dhamana.”
Kufikia jana Jumanne, maafisa wanaoendeleza operesheni ya ufukuaji kutafuta maiti zaidi za wahanga wa imani potofu za mchungaji huyo wa kanisa la Good News International walikuwa wamefanikiwa kufukua maiti za watu 133 katika shamba lake huko Shakahola.

Tayari Rais William Ruto wa Kenya ameunda tume itakayochunguza mauaji hayo tata katika msitu wa Shakahola ambao uko katika shamba linalomilikiwa na kasisi aliyehusishwa na mauaji hayo. Wakili Kioko Kilukumi ataongoza wakili mkuu na kusaidiwa na Vivian Nyambeki na Bahati Mwamuye.
Tume hiyo itachunguza vifo vya zaidi ya watu 130 wanaoaminika kuwa ni wafuasi wa pote hilo la Kikristo lenye misimamo mikali ambalo kiongozi wake aliwaamuru wakae na njaa hadi kufa ili waweze kukutana na Yesu mbinguni.
Kulingana na notisi iliyotolewa kwenye gazeti la serikali, tume hiyo itatayarisha ripoti chini ya miezi sita na kutoa mapendekezo yao kwa Rais Ruto. Tume hiyo ina jukumu la kubainisha chanzo cha vifo vilivyotokea na pia kuchunguza ni nini kilichosababisha idara za usalama, usimamizi na sheria kufeli kuchukua hatua hadi maafa kutokea.