Watu 11 wauawa katika hujuma ya wanamgambo magharibi mwa Kongo
(last modified Sun, 14 May 2023 06:54:13 GMT )
May 14, 2023 06:54 UTC
  • Watu 11 wauawa katika hujuma ya wanamgambo magharibi mwa Kongo

Watu wasiopungua 11 wameuawa katika hujuma ya wanamgambo wenye silaha magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Haya ni kwa mujibu wa maafisa wa Kongo.

Adelar Nkisi Msemaji wa serikali ya jimbo ameeleza kuwa, wanamgambo kwa jina la "Mobondo" kutoka jamii ya Yaka walikivamia kijiji cha Batshongo katika jimbo la Kwango na kuuwa wanajeshi wawili, afisa polisi mmoja na raia wawili. Ameongeza kuwa,  askari hao wameuliwa kwa kukatwa vipande vipande. 

Mapigano yalizuka huko Batshongo juzi usiku na kuendelea hadi jana Jumamosi huko Mongata kijiji kilichoko umbali wa kilomita 8 magharibi mwa makao makuu ya kijimbo ya mji mkuu Kinshasa. Msemaji wa serikali ya jimbo la Kwango ameeleza kuwa, serikali ya jimbo hilo ilitangaza muda wa kutotoka nje kuanzia saa mbili usiku hadi leo asubuhi. 

Wakati huo huo Symphorien Kwengo kiongozi wa taasisi ya kiraia ya Kwango ameeleza kuwa watu wanane wameuawa huko Batshingo na 11 huko Mongata. Machafuko katika mikoa ya magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yaliibuka kwa mara ya kwanza katika eneo la Kwamouth katika jimbo la Mai-Ndombe katika mzozo wa zaka ya kimila kati ya jamii za Teke na Yaka.

Tags