Mhandisi, walinzi wa mbunga ya Virunga wauawa katika shambulio la waasi DRC
(last modified Fri, 19 May 2023 08:31:20 GMT )
May 19, 2023 08:31 UTC
  • Mhandisi, walinzi wa mbunga ya Virunga wauawa katika shambulio la waasi DRC

Mhandisi na walinzi watatu wa hifadhi ya wanyama pori ya Virunga wameuawa katika shambulio la kuvizia lililofanywa na watu wenye silaha dhidi ya msafara wao karibu na Mbuga ya Kitaifa ya Virunga Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Taarifa iliyotolewa na Taasisi ya Hifadhi ya Mazingira ya Congo (ICCN) imesema kuwa wanamgambo wanaodaiwa kuwa wa "Mai-Mai" waliuvamia msafara wa mafundi waliopewa zabuni ya miradi ya maendeleo katika eneo la Lubero (jimbo la Kivu Kaskazini) Alhamisi asubuhi.

Shambulizi hilo limefanyika wakati msafara huo ulipokuwa ukisindikizwa na walinzi wa ICCN kutoka kijiji cha Kivandya karibu na hifadhi ya Virunga, wanakopatikana sokwe wa milimani walio hatarini kutoweka.

Mkuu wa wilaya ya Lubero, Kanali Alain Kiwewa Mitela, amethibitisha kuwa walinzi watatu na mtaalamu wa kiufundi waliuawa na wengine sita wamejeruhiwa.

Eneo hilo limekuwa likiathiriwa na mashambulio ya mara kwa mara ya wanamgambo wenye silaha.

Virunga ndio hifadhi ya zamani zaidi barani Afrika na hifadhi maarufu ya wanyama adimu, kama vile sokwe wa milimani.

Sokwe wa mbunga ya Virunga

Eneo hilo pia ni linatambuliwa kuwa maficho ya wanamgambo wa Mai Mai.

Tags