Bola Tinubu aapishwa kuwa Rais mpya wa Nigeria
Bola Ahmed Tinubu ameapishwa kuwa Rais wa tano wa Nigeria tokea kurejea kwa utawala wa demokrasia nchini humo mwaka 1999; huku akiwahijiwa na changamoto nyingi za kiuchumi na kiusalama.
Tinubu ameapishwa leo Jumatatu na Olukayode Ariwoola, Jaji Mkuu wa nchi hiyo katika hafla iliyofanyika Abuja, mji mkuu wa Nigeria, na kuhudhuriwa na marais na viongozi mbalimbali hasa wa Afrika.
Bola Tinubu mwenye umri wa miaka 71 anarithi mikoba ya Muhammadu Buhari, ambaye sheria ilimbana kugombea muhula mwingine, baada ya kuongoza kwa mihula miwili tokea 2015.
Tinubu anakabiliwa na changamoto nyingi wakati huu anapomrithi Buhari (80) ambaye kipindi chake cha uongozi kilikabiliwa na ukosoaji mkubwa.
Ataliongoza taifa ambalo asilimia 63 ya watu ni maskini, huku asilimia 33 wakiwa hawana ajira. Aidha nchi hiyo inasumbuliwa na ukosefu wa usalama kutokana na mashambulizi ya magenge ya kigaidi ya Boko Haram, utekaji nyara na mapigano ya kikabila.
Tinubu alitangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais uliofanyika Machi mwaka huu. Tume Huru ya Uchaguzi Nigeria (INEC) ilimtangaza Tinubu aliyegombea kupitia chama tawala cha All Progressives Congress (APC) kuwa mshindi wa uchaguzi urais, kwa kupata kura milioni 8.8, akifuatiwa na mshindani wake wa karibu Atiku Abubakar wa chama cha Peoples Democratic Party (PDP) aliyepata kura milioni 6.9.