DRC: Jeshi la Sudan limeua raia wetu 10 mjini Khartoum
(last modified Tue, 06 Jun 2023 06:32:36 GMT )
Jun 06, 2023 06:32 UTC
  • DRC: Jeshi la Sudan limeua raia wetu 10 mjini Khartoum

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imesema raia kumi wa nchi hiyo wameuawa katika mashambulizi ya Jeshi la Sudan ndani ya Chuo Kikuu kimoja mjini Khartoum, huku mapigano yakishtadi nchini Sudan kati ya jeshi na wapiganaji wa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF).

Waziri wa Mambo ya Nje wa Kongo DR, Christophe Lutundula ameviambia vyombo vya habari kuwa, mashambulizi ya mabomu ya Jeshi la Sudan siku ya Jumapili yaliua Wakongomani kumi, kwenye bewa la Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Afrika (IUA) jijini Khartoum.

Lutundula amesema jana Jumatatu alimuita ofisini Naibu Balozi wa Sudan mjini Kinshasa, ili kumkabidhi ujumbe wa malalamiko ya serikali ya DRC juu ya mauaji hayo ya raia wa nchi hiyo jijini Khartoum. Amesema Kinshasa imesikitishwa na mauaji hayo.

Huku hayo yakiripotiwa, jeshi la Sudan limedai kuwa limekomboa kambi ya Jeshi la Anga mjini Khartoum baada ya mapigano makali na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF); huku wapiganaji hasimu wakidai kuwa wameteka ngome ya kijeshi ya magharibi mwa nchi hiyo.

Mapigano Sudan

Taarifa zinasema, tangu mzozo kati ya majenerali wawili hasimu wa Sudan ulipozuka Aprili 15, zaidi ya watu 1,800 wameuawa mbali na wengine zaidi ya milioni moja wakilazimika kuyahama makazi yao na kuwa wakimbizi.

Hata hivyo  madaktari na mashirika ya misaada yanasema, idadi halisi ya watu waliouawa inakadiriwa kuwa kubwa zaidi, ikitiliwa maanani idadi ya miili iliyoachwa katika maeneo ambayo hayakuweza kufikiwa.

Tags