Viongozi wa Igad wanakutana leo Djibouti kujadili mapigano ya ndani Sudan
Jumuiya ya Maendeleo ya Kiserikali (IGAD) inafanya mkutano wa kilele nchini Djibouti leo Jumatatu ili kuzishawishi pande mbili katika mgogoro wa Sudan kufanya mazungumzo ya kumaliza mapigano ya wenyewe kwa wenyewe, wakati huu ambapo mji mkuu Khartoum unashuhudia mapigano makali.
Kabla ya mkutano wa leo wa IGAD, Djibouti ilikuwa mwenyeji wa mkutano mdogo wa jumuiya hiyo hapo jana, uliowakutanisha pamoja marais wa Sudan Kusini, Salva Kiir Mayardit, William Ruto wa Kenya na Ismail Omar Guelleh wa Djibouti.
Rais wa Djibouti alisema kuwa nchi za IGAD zitachunguza njia za kulishawishi jeshi la Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka kufanya mazungumzo ambayo yatahakikisha usitishaji vita, na alieleza wasiwasi wake mkubwa juu ya athari mbaya za mzozo wa vita nchini Sudan.
Kwa upande wake, Rais William Ruto wa Kenya ameitaja hali ya Sudan kuwa mbaya na inazidi kuwa tata, akitoa wito kwa viongozi wa shirika la IGAD kukomesha vita vinavyoendelea nchini huumo. Rais Ruto amesisitiza udharura wa viongozi wa IGAD kukubaliana juu ya suala la kusitisha vita nchini Sudan na kuziwezesha pande mbili kufanya mazungumzo kuhusu mustakabali wa Sudan.
Katika mkutano wake wa kilele wa dharura Aprili mwaka jana, IGAD iliidhinisha Djibouti, Sudan Kusini na Kenya kufanya mawasiliano ili kusitisha mapigano nchini Sudan.
Wakati huo huo ripoti zinasema kuwa, mapigano makali na makabiliano ya silaha nzito yalizuka jana Jumapili kati ya jeshi na Vikosi vya Msaada wa Haraka katika maeneo kadhaa ya miji ya Khartoum na Omdurman.
Katika upande mwingine Muungano wa Madaktari wa Sudan umesema kwamba mji wa El Geneina (katikati ya jimbo la Darfur Magharibi kwenye mpaka na Chad) umegeuka kuwa "mji wa mizimu, usio na chochote ila harufu ya kifo."
Tangu Aprili 20, mji huo umekuwa ikishuhudia mashambulizi ya mfululizo ya makabila yanayohusishwa na Vikosi vya Msaada wa Haraka ambayo yamesababisha vifo vya mamia ya watu na kuwalazimisha maelfu ya wengine kuwa wakimbizi.