AU yaonya kuhusu matokeo mabaya ya kuendelea mapigano Sudan
Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) ameonya juu ya matokeo mabaya ya kuendelea vita na mapigano nchini Sudan. Mapigano hayo ni baina ya jeshi la Sudan linaloongozwa na Abdel Fattah al Burhan, na vikosi vya Usaidizi wa Haraka (RSF) chini ya uongozi wa Muhammad Hamdan Daghalo Kamanda.
Moussa Faki Mahamat ametoa indhari hiyo katika mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kiserikali (IGAD) unaofanyika nchini Djibouti kujadili mgogoro wa Sudan na kueleza kuwa, iwapo mapigano hayo hayatasitishwa, kuna uwezekano wa kuibuka mapinduzi ya ndani.
Faki Mahamat amesema mgogoro wa Sudan si tu unahataisha uwepo wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika, bali eneo hilo zima.
Viongozi wa jumuiya ya kieneo ya mashariki mwa Afrika IGAD wamebainisha masikitiko yao kwa kuendelea kukiukwa mara kwa mara makubaliano ya kusitisha vita jiji Khartoum na katika maeneo mengine ya nchi hiyo ya Kiarabu.
Mkutano wa IGAD umefanyika huku mapigano yakishtadi katika maeneo mbalimbali ya Khartoum, mji mkuu wa Sudan, baada ya kumalizika kwa makubaliano ya usitishaji vita kwa muda wa saa 24.
Kabla ya mkutano wa leo wa IGAD, Djibouti ilikuwa mwenyeji wa mkutano mdogo wa jumuiya hiyo ya kikanda hapo jana, uliowakutanisha pamoja marais wa Sudan Kusini, Salva Kiir Mayardit, William Ruto wa Kenya na Ismail Omar Guelleh wa Djibouti.
Mapigano ya ndani Sudan mbali na kusababisha vifo vya watu 1,800, lakini pia yamewalazimisha watu zaidi ya milioni moja na laki mbili kuwa wakimbizi ndani ya nchi hiyo, huku wengine karibu ya laki nne wakikimbilia katika nchi jirani.