Jeshi la Uganda limeanza kuwasaka wahalifu ili kuwaokoa wanafunzi waliotekwa nyara
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i98932-jeshi_la_uganda_limeanza_kuwasaka_wahalifu_ili_kuwaokoa_wanafunzi_waliotekwa_nyara
Uganda imeimarisha ulinzi na tayari imeanzisha msako mkubwa baada ya wanamgambo wenye silaha wa ADF wenye mfungamano na kundi la kigaidi ya Daesh (ISIS) kuwauwa watu wasiopungua 41; wengi wao wakiwa ni wanafunzi. Mauaji hayo yamefanyika katika maeneo ya Magharibi mwa Uganda karibu na mpaka na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 18, 2023 06:53 UTC
  • Jeshi la Uganda limeanza kuwasaka wahalifu ili kuwaokoa wanafunzi waliotekwa nyara

Uganda imeimarisha ulinzi na tayari imeanzisha msako mkubwa baada ya wanamgambo wenye silaha wa ADF wenye mfungamano na kundi la kigaidi ya Daesh (ISIS) kuwauwa watu wasiopungua 41; wengi wao wakiwa ni wanafunzi. Mauaji hayo yamefanyika katika maeneo ya Magharibi mwa Uganda karibu na mpaka na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Akitoa taarifa kuhusu hali ya mambo huko Uganda, Bi Janet Museveni, mke wa Rais Yoweri Museveni wa nchi hiyo ambaye ni Waziri wa Elimu na Michezo amesema kuwa serikali ingali inachunguza tukio zima. Amesema serikali ya Uganda, kupitia idara za usalama, inajaribu kufuatilia kilichotokea na kwamba wanaamini kuwa sheria itafuata mkondo wake. 

Maafisa na watu walioshuhudia tukkio hilo wameeleza kuwa bunduki na visu vilitumiwa  katika shambulio la usiku wa manane kuamkia jana Jumamosi huku mabweni ya Shule ya Sekondari ya Lubiriha iliyopo Mpondwe magharibi mwa Uganda, yakitekezwa kwa moto.

Baadhi ya wanafunzi walionusurika na mauaji hayo wamesimulia tukio hilo wakilitaja kuwa la kutisha. Wamesema usiku huo wa kuamkia Jumamosi ya jana walikuwa bado hawajalala ambapo walisikia watu wakiwasili katika mabweni yao wakisema, fungua, fungua, na kwamba walianza kufyatua risasi madirishani na kwenye milango. 

Magaidi wa ADF washambulia shule Uganda na kuuwa watu 41 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ameleani vikali shambulizi hilo lililofanywa na wanamgambo wa ADF na kutoa mkono wa pole na taazia kwa familia ya wahanga wa mauaji hayo. Guterres amesema wale waliohusika na jinai hiyo ya kutisha lazima wafikishwe kwenye vyombo vya sheria. 

Wakati huo huo Felix Kulayigye Msemaji wa Vikosi vya Ulinzi vya Uganda (UPDF) amesema mateka sita wamepelekwa katika Mbuga ya Taifa ya Virunga na kwamba vikosi hivyo vimeanza kuwasaka wahalifu ili kuwakomboa wanafunzi waliotekwa nyara.