Kinara wa upinzani DRC atishia kususia uchaguzi wa rais wa Disemba
(last modified Wed, 21 Jun 2023 03:44:57 GMT )
Jun 21, 2023 03:44 UTC
  • Kinara wa upinzani DRC atishia kususia uchaguzi wa rais wa Disemba

Martin Fayulu, kiongozi wa upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ametishia kuwa huenda asishiriki uchaguzi mkuu ujao, huku mvutano wa kisiasa ukiongezeka nchini humo kabla ya uchaguzi wa rais wa Disemba 20, ambapo Rais Felix Tshisekedi anatarajiwa kugombea muhula wa pili.

Fayulu ambaye ni kinara wa chama cha Engagement for Citizenship and Development amesema chama chake hakitashiriki katika uchaguzi huo wa Disemba, iwapo daftari la wapiga kura halitakaguliwa na kupigwa msasa.

Kwa mujibu wa matokeo rasmi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini humo CENI, Fayulu aliibuka wa pili katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2018, akibwagwa na Rais wa sasa wa nchi hiyo, Felix Tshisekedi. Kesi yake ya kupinga matokeo hayo ilitupiliwa mbali na mahakama.

Tume ya CENI imeandikisha karibu wapiga kura milioni 43.9 kwa aili ya uchaguzi mkuu wa mwezi Disemba, ikilinganishwa na milioni 40.4 katika uchaguzi uliopita. 

Viongozi wa upinzani wametilia shaka idadi ya waliojiandikisha kupiga kura wakisema hakukuwa na ukaguzi huru wa orodha ya wapiga kura katika nchi hiyo kubwa ya katikati mwa Afrika yenye watu  zaidi ya milioni 95.

Fayulu amewaambia waandishi wa habari mjini Kinshasa kuwa, "Kila mmoja anafahamu kuwa mchakato wa kuwatambua na kuwasajili wapiga kura haukuwa na uwazi, na hiyo ni ithibati ya kuwepo njama za kuiba kura."

Wagombea wa ubunge nchini humo wana hadi Juni 25 kuwasilisha majina yao kwa CENI, huku wagombea wa urais wakiwa na fursa ya hadi mwezi Septemba kuwasilisha maombi yao rasmi ya kuwania kiti hicho.

Tags